Na Lucy Lyatuu,Dodoma
SERIKALI imezindua kituo cha Kubadilishia Njia za Usambazaji Umeme (Switching Station) pamoja na Transforma ya Kudhibiti Umeme (AVR) ikiwa ni sehemu muhimu ya jitihada za za kuimarisha uthabiti wa mfumo wa usambazaji wa umeme na kuongeza uhakika wa huduma kwa wananchi.
Akizindua kituo hicho mkoani hapa katika wilaya ya Kongwa , WAZIRI wa Nishati, Deogratius Ndejembi amesema kupitia uwekezaji wa Serikali wa zaidi ya sh bilioni 10.5, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imefanikiwa kujenga Kituo cha Kubadilishia Njia za Usambazaji Umeme.
Amesema ujenzi huo pia umehusisha kusimika Transforma ya Kudhibiti Umeme yenye uwezo wa MVA 20 pamoja na miundombinu mingine ikiwemo njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 kutoka Zuzu hadi Mbande yenye urefu wa kilomita 92.

Ndejembi amesema Serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini.
Aidha amesema Serikali inaendelea na mipango mbalimbali ya kuongeza uwezo huo ili kufikia zaidi ya megawati 8,000 katika miaka ijayo pamoja na mahitaji ya maendeleo ya Taifa na matarajio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Amesema kutokana na umuhimu huo, Serikali imeendelea kuupa Mkoa huo kipaumbele maalum katika uwekezaji wa miundombinu ya nishati ili kuhakikisha huduma ya umeme inakuwa ya uhakika, salama na yenye viwango vinavyokidhi mahitaji ya taasisi za Serikali, sekta binafsi, wawekezaji na wananchi kwa ujumla.

“Kwa kutambua ukuaji wa haraka wa Mkoa wa Dodoma na ongezeko la mahitaji ya huduma ya umeme, Wizara ya Nishati kupitia TANESCO imeendelea kuharakisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kuimarisha usafirishaji na usambazaji wa umeme mkoani hapa,” amesema.
Amesema lengo ni kuona Mkoa wa Dodoma unaendelea kuwa mfano wa upatikanaji wa huduma bora za umeme zinazowezesha utoaji wa huduma za Serikali, ukuaji wa biashara, uwekezaji wa viwanda na maendeleo ya kijamii yanayostahili Makao Makuu ya Taifa.
Amesema ni katika muktadha huo ndipo Serikali ilipoidhinisha utekelezaji wa mradi tunaouzindua leo hapa Mbande.
Amesema Kwa muda mrefu, wananchi wa Wilaya ya Kongwa walitegemea njia moja ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 kutoka Dodoma Mjini, hali iliyokuwa ikisababisha changamoto za upatikanaji wa umeme wa uhakika kutokana na ongezeko la mahitaji ya huduma hiyo.
Amesema Kukamilika kwa miundombinu hii kutaimarisha upatikanaji wa huduma ya umeme katika Wilaya za Kongwa, Gairo, Chamwino pamoja na baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Mpwapwa.

Kwa wananchi wa Kongwa na maeneo yote yanayonufaika na mradi huu, ninawahimiza kuendelea kuitunza miundombinu hii na kutumia fursa ya upatikanaji wa umeme wa uhakika kuongeza uzalishaji, kukuza biashara na kuboresha maisha yao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Wa TANESCO,Lazaro Twange amesema uzinduzi huo ni muhimu kwa wananchi wa Wilaya za Kongwa, Chamwino,Gairo,na baadhi ya maeneo ya Mpwapwa katika Mkoa wa Dodoma kwa ujumla.
Amesema hayo ni matokeo ya uwekezaji wa Serikali katika kuimarisha miundombinu ya usambazaji wa umeme na kuongeza uhakika wa huduma kwa wananchi.
Amesema Shirika limeendelea kufanya tathmini ya mahitaji ya huduma ya umeme katika maeneo mbalimbali nchini na kuandaa miradi ya kimkakati inayolenga kuimarisha mfumo wa usafirishaji na usambazaji wa umeme.
“Kupitia tathmini hizo, ilibainika kuwa pamoja na ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii katika Wilaya ya Kongwa na maeneo jirani, kulikuwa na haja ya kuimarisha uthabiti wa mfumo wa usambazaji wa umeme ili kuendana na ongezeko la mahitaji ya huduma hiyo.,” amesema.
Amesema Kwa muda mrefu, wananchi wa Kongwa walitegemea njia moja ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 kutoka Dodoma Mjini, hali iliyokuwa ikisababisha changamoto za upatikanaji wa umeme wa uhakika hususan wakati wa matengenezo au hitilafu za kiufundi.

Amesema Kutokana na hali hiyo, TANESCO iliona umuhimu wa kuwekeza katika miundombinu itakayoongeza uwezo wa mfumo wa usambazaji wa umeme, kuboresha viwango vya huduma na kuweka mazingira bora ya maendeleo kwa wananchi wa Kongwa na maeneo jirani.
Amesemaiundombinu hiyo itatoa uthabiti wa mfumo wa usambazaji wa umeme, kupunguza athari za hitilafu, kuboresha viwango vya umeme na kuongeza uwezo wa TANESCO kuhudumia wateja waliopo pamoja na mahitaji yatakayojitokeza katika siku zijazo.

