Na Lucy Ngowi
MIAKA michache iliyopita, wengi walitazama Kiswahili kama lugha ya mawasiliano ya Afrika Mashariki pekee.
Leo hali imebadilika kwa kasi kubwa. Lugha hiyo sasa inafundishwa katika vyuo vikuu duniani, inatumika katika taasisi za kimataifa na imekuwa daraja linalounganisha mataifa, tamaduni na fursa za kiuchumi.

Ukuaji huo unadhihirishwa na kufanyika kwa Kongamano la Pili la Kiswahili la Kimataifa, litakalofanyika katika Makao Makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) jijini Paris, Ufaransa, kuanzia Julai 4 Duniani.mwaka huu 2026, sambamba na Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani.
Kwa Tanzania, ambayo ndiyo chimbuko na ngome ya Kiswahili duniani, kongamano hilo si tukio la kawaida.
Ni hatua muhimu katika safari ya kuifanya lugha hiyo kuwa nyenzo ya maendeleo ya kiuchumi, diplomasia na ajira kwa vijana kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Consolata Mushi, anasema Tanzania ina nafasi ya kipekee ya kunufaika na ongezeko la matumizi ya Kiswahili duniani kupitia elimu, tafsiri, teknolojia za lugha, utalii wa utamaduni, sanaa, vyombo vya habari na maudhui ya kidijiti.

Anabainisha kuwa Serikali imeendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Kubidhaisha Kiswahili wa miaka 10 uliozinduliwa mwaka 2022.
Mkakati huo unalenga kukuza taaluma za Kiswahili, kuimarisha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia lugha hiyo, kuongeza machapisho ya Kiswahili na kupanua huduma za tafsiri, ukalimani, uhariri, ufundishaji na utangazaji.
Anasema hatua hizo zimefungua milango ya ajira kwa walimu, watafiti, waandishi, wataalamu wa lugha na vijana wenye ujuzi wa teknolojia.
Mafanikio ya juhudi hizo tayari yanaonekana.
Kongamano la Kwanza la Kiswahili la Kimataifa lililofanyika Havana, Cuba, mwaka 2024 lilifanikiwa kupanua matumizi ya Kiswahili katika nchi zinazozungumza Kihispania.
Leo, Kiswahili kinafundishwa katika Chuo Kikuu cha Havana kupitia ushirikiano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, huku vitabu na kamusi zilizoandaliwa Tanzania zikitumika kufundishia lugha hiyo.
Kadiri idadi ya watu wanaojifunza Kiswahili duniani inavyoongezeka, ndivyo mahitaji ya vitabu, kamusi, huduma za tafsiri na mafunzo ya lugha yanavyokua.
Hii inaifanya lugha hiyo kuwa rasilimali yenye thamani kubwa ya kiuchumi.
Mbali na huduma za lugha, Kiswahili kimeendelea kuwa injini ya uchumi wa ubunifu.
Filamu, muziki, tamthilia, vitabu, michezo ya kidijiti na maudhui ya mtandaoni yanayotumia Kiswahili yanapata watazamaji na watumiaji wengi zaidi duniani, hali inayochangia kuongeza mapato na kuitangaza Tanzania kimataifa.
Kwa upande wa diplomasia, Kiswahili kimeendelea kupata hadhi kubwa katika taasisi za kikanda na kimataifa.
Kwa sasa ni lugha rasmi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU), UNESCO na taasisi nyingine za kimataifa.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliwahi kueleza kuwa Kiswahili si lugha ya mawasiliano pekee, bali ni nyenzo muhimu ya diplomasia, utamaduni na mshikamano inayowaunganisha watu na kuchochea maendeleo endelevu.

Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, alisema Kongamano la Paris ni tukio la kihistoria linaloendelea kuthibitisha nafasi ya Tanzania na Bara la Afrika katika kukuza na kueneza Kiswahili duniani.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, kaulimbiu ya kongamano hilo ni “Kiswahili kwa Amani, Mshikamano na Diplomasia ya Uchumi Duniani.”
Kaulimbiu hiyo inaakisi dhamira ya kutumia Kiswahili kama chachu ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa miongoni mwa mataifa.
Wakati dunia ikiingia zaidi katika zama za teknolojia na akili unde (AI), wataalamu wanaona Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha zenye fursa kubwa za kukua kupitia mifumo ya tafsiri, programu za kujifunzia lugha mtandaoni na maendeleo ya teknolojia za lugha.
Kwa mtazamo huo, Kongamano la Paris halitakuwa tu mkutano wa wataalamu wa lugha.
Litakuwa jukwaa la kuonesha namna Kiswahili kinavyoweza kuwa daraja la maarifa, biashara, ajira na ushawishi wa kidiplomasia duniani.
Kwa hakika, safari ya Kiswahili imevuka mipaka ya Afrika Mashariki. Kutoka Dar es Salaam hadi Paris, lugha hii inaendelea kuandika historia mpya na kuthibitisha kuwa urithi wa Afrika unaweza kuwa nguvu ya maendeleo ya dunia nzima.

