Na Lucy Lyatuu, Dodoma
MAMLAKA Ya Udhibiti Mkondo Wa Juu Wa Petroli (PURA) Tanzania imeanza shughuli ya kutafuta mafuta tangu mwaka 1950 na imechimba visima zaidi ya 97, lakini bado nchi haijafanikiwa kupata mafuta ya kibiashara, lakini imefanikiwa kugundua gesi asilia ambayo inaendelea kutumika katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mhandisi Charles Sangweni amesema kuwa Tanzania inaendelea kujivunia uwepo wa akiba kubwa ya gesi asilia ambayo imekuwa nguzo muhimu katika maendeleo ya sekta ya nishati na uchumi wa taifa.
Akizungumza katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma Jijini Dodoma, Sangweni amesema kuwa PURA imeendelea kusimamia shughuli za utafutaji, uchimbaji na maendeleo ya rasilimali za mafuta na gesi kwa mujibu wa sheria na miongozo ya nchi.
Aidha, amebainisha kuwa matumizi ya gesi asilia yanaendelea kuongezeka duniani kutokana na mabadiliko ya teknolojia na juhudi za kupunguza matumizi ya nishati zinazochafua mazingira, hali inayofanya rasilimali hiyo kuwa na umuhimu mkubwa kwa Tanzania.
Ameongeza kuwa Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, jambo linaloongeza mahitaji ya gesi asilia na kutoa fursa zaidi za uwekezaji katika sekta hiyo.
Sangweni amesema kuwa PURA imeendelea kuhakikisha Watanzania wananufaika na rasilimali za petroli kupitia ajira, utoaji wa huduma na bidhaa pamoja na ushirikishwaji katika miradi mbalimbali chini ya sera ya Local Content.
Aidha, amebainisha kuwa mamlaka hiyo imeanzisha mifumo ya kuwaunganisha wataalamu wa Kitanzania na wawekezaji ili kuongeza ajira na kukuza uwezo wa wazawa kushiriki kikamilifu katika sekta ya mafuta na gesi.
Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya utafutaji wa mafuta na gesi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Eyasi Wembere pamoja na vitalu vya Lindi na Mtwara vinavyotekelezwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Kuhusu changamoto za mabadiliko ya bei ya mafuta duniani, Sangweni amesema kuwa Tanzania imeendelea kuwa katika hali nzuri ya upatikanaji wa mafuta licha ya migogoro ya kimataifa inayotokea katika baadhi ya maeneo ya dunia.
Amebainisha kuwa nchi za Afrika Mashariki na Kati zimeendelea kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika matumizi na usambazaji wa rasilimali za nishati ili kuhakikisha usalama wa nishati kwa wananchi hata wakati wa changamoto za kimataifa.
Amesema Afrika inapaswa kuendelea kutumia rasilimali zake za mafuta, gesi na madini kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wake huku ikiendelea kuzingatia masuala ya utunzaji wa mazingira.

