Na Lucy Ngowi
DODOMA: NAIBU Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Qwaray, ameipongeza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa mchango wake katika kuwajengea vijana ujuzi unaowawezesha kujiajiri na kuchangia maendeleo ya uchumi wa nchi.
Akizungumza baada ya kutembelea banda la VETA katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma Juni 22, 2026, Qwaray amesema Serikali imejikita katika kuwawezesha vijana kujiajiri, jambo ambalo litafanikiwa zaidi kupitia uwekezaji mkubwa katika elimu ya ufundi na stadi za kazi.
“Vijana wanapopata ujuzi wa ufundi wanakuwa na uwezo wa kujitegemea kiuchumi badala ya kusubiri ajira za Serikali. Hivyo, ni muhimu kuendelea kuwekeza katika vyuo vya VETA ili kuongeza fursa za ajira na uzalishaji,” amesema.

Qwaray pia ameipongeza VETA kwa kutoa mafunzo kwa watu wenye mahitaji maalum na kwa juhudi zake za kuzalisha bidhaa mbalimbali kupitia kampuni tanzu ya VETA Ujuzi, hatua inayochangia kukuza uchumi na kuongeza thamani ya mafunzo yanayotolewa.
Amesema wahitimu wa elimu mbalimbali, ikiwemo kidato cha nne na elimu ya juu, wanapaswa kutumia fursa zinazotolewa na VETA kupata stadi zinazowawezesha kujiajiri na kuanzisha shughuli za uzalishaji.
Aidha, amebainisha kuwa maendeleo ya ujuzi kwa wananchi ni nguzo muhimu katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi wa kisasa unaotegemea maarifa na ubunifu.

VETA ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyoanza Juni 16, 2026, kufunguliwa rasmi Juni 17 na Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, na yanatarajiwa kuhitimishwa Juni 23, 2026.

