Na Lucy Lyatuu,Dodoma
BALOZI wa Tanzania nchini Italia na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Mashirika ya Umoja wa Mataifa ya FAO, WFP na IFAD, Mbarouk Nassor Mbarouk, ametembelea Banda la Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) katika Maonesho ya Nane Nane yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma, ambapo amejionea bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na vikundi vya wakulima na wafugaji.

Katika ziara hiyo, Balozi Mbarouk amezungumza na wataalamu wa FAO kutoka idara mbalimbali kuhusu shughuli zinazotekelezwa na shirika hilo nchini.
FAO ni Shirika la Umoja wa Mataifa linaloongoza juhudi za kupambana na njaa na kuboresha mifumo ya chakula, likishirikiana na Serikali na wadau katika kuendeleza kilimo, mifugo, uvuvi na kuongeza uzalishaji na kipato cha wananchi.

Balozi Mbarouk ameipongeza FAO kwa utendaji kazi wake na mchango wake katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuleta maendeleo nchini, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, FAO na wadau mbalimbali katika kukuza sekta za uzalishaji na kuboresha maisha ya wananchi.

