Na Lucy Ngowi
Kwa mkulima wa maharage, madoa yanapoanza kutanda kwenye majani si tatizo dogo. Ni ishara ya ugonjwa unaoweza kupunguza uzalishaji na kuathiri ubora wa mazao.
Mkulima kutoka Mbeya, Yusta Mwakibona, anasema ugonjwa wa doa pembe hushambulia majani ya maharage na kupunguza uwezo wa mmea kutengeneza chakula.
“Ugonjwa unaposhambulia majani, mmea unapoteza uwezo wa kutengeneza chakula. Majani hukauka na kudondoka, jambo ambalo hupunguza uzalishaji na kushusha ubora wa mazao,” anasema.
Utafiti uliofanyika Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania unaonyesha ukubwa wa changamoto hiyo, ukibainisha kuwa katika mazingira yenye mvua nyingi, mashamba yasiyodhibiti ugonjwa wa doa pembe yanaweza kupata hasara ya mavuno hadi asilimia 61.
Changamoto hiyo ina uzito katika nchi ambayo maharage ni zao muhimu la chakula na kipato. Kwa mujibu wa Taarifa ya Mwaka ya Kilimo 2023/24, Tanzania ilizalisha takribani tani milioni 1.68 za maharage, ikionyesha umuhimu wa kulinda uzalishaji wa zao hilo.
Ni katika mazingira hayo ambapo utafiti wa Dkt. Luseko Chilagane, mtafiti wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), unatafuta suluhisho la muda mrefu, mbegu zenye uwezo wa kustahimili ugonjwa huku zikibaki na sifa zinazopendwa na wakulima na walaji.
Utafiti huo umewezeshwa kwa Sh. Milioni 70 kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).

Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Dkt. Luseko Chilagane, akionesha sampuli ya maharage kwa watafiti kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) wakati wa ziara yao katika moja ya maabara za chuo hicho. Wa kwanza kulia ni Dkt. Bunini Manyilizu, akifuatiwa na Dkt. Deogracious Protas.
UWEKEZAJI KATIKA UTAFITI WA KIMKAKATI
Ofisa Mwandamizi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kupitia Mfuko wa Taifa wa Uendelezaji wa Sayansi na Teknolojia (MTUSATE), Ntufye Mwakigonja, anasema uwekezaji huo ulitokana na mpango maalumu wa kuwaimarisha watafiti wachanga baada ya shahada ya uzamivu.
Anasema COSTECH ilitengeneza mwongozo mahsusi wa kuwaimarisha watafiti hao kupitia Postdoctoral Development Programme, ambapo Tume ilitenga Sh. Milioni 420 kwa ajili ya kuwaimarisha watafiti sita baada ya shahada ya uzamivu.
Dkt. Luseko Chilagane alikuwa miongoni mwa watafiti hao, huku Sh. Milioni 70 zikitumika kugharamia utafiti uliolenga kutafuta suluhisho la ugonjwa wa doa pembe katika zao la maharage.
“COSTECH inaweka mkazo katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazokabili jamii kupitia utafiti wa kimkakati,” anasema Ntufye.
KUTOKA VINAASABA VYA KIENYEJI
Dkt. Chilagane alilenga kutumia vinasaba kutoka kwenye mbegu za maharage ya kienyeji zenye ukinzani dhidi ya doa pembe na kuvihamishia kwenye aina zinazopendwa zaidi sokoni.
Doa pembe, inayojulikana pia kama ‘Angular Leaf Spot (ALS)’, husababisha madoa kwenye majani na kupunguza eneo la kijani linalohusika na utengenezaji wa chakula cha mmea. Tatizo huwa kubwa zaidi katika maeneo yenye unyevunyevu na baridi, yakiwamo baadhi ya maeneo ya Mbeya, Arusha na Mgeta mkoani Morogoro.
Kwa hiyo, lengo halikuwa kutengeneza maharage yanayostahimili ugonjwa pekee, bali kupata mchanganyiko wa ukinzani wa ugonjwa, mavuno na sifa zinazokubalika sokoni.
SAYANSI INAKUTANA NA SOKO
Utafiti ulijikita pia kwenye aina zinazopendwa na walaji, hususan maharage ya njano yanayojulikana kama “Njano golori” na ya kijivu yanayojulikana kama “Kablanketi”.
Kwa mujibu wa Reinfrid Maganga, mratibu wa zao la maharage kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), aina hizo hupendwa kwa sababu ya ladha na sifa nyingine zinazokubalika kwa walaji.
Katika mchakato huo, utafiti umefikia kupata aina za awali 18 za maharage yenye wazazi tofauti. Baadhi ya aina hizo zimeonyesha ukinzani dhidi ya doa pembe, huku pia zikiunganisha sifa zinazopendwa kutoka aina ya Njano na Kijivu.
Hata hivyo, hapa ndipo umuhimu wa kutofautisha matokeo ya utafiti na mbegu zilizo tayari kwa matumizi ya wakulima unapojitokeza.
Aina hizo za awali 18 bado si aina za mbegu zilizoidhinishwa kwa matumizi ya wakulima. Aina hizi za awali zipo katika hatua ya utafiti na uchaguzi. Hatua inayofuata ni kufanya majaribio na uthibitishaji kwa kushirikina na wakulima katika mazingira ya wakulima ili kutathmini ukinzani dhidi ya ugonjwa, mavuno na sifa zinazopendwa na walaji kabla ya kufikia hatua ya kuidhinishwa.
LENGO NI MAVUNO ZAIDI
Kwa mazingira ambayo uzalishaji unaweza kuwa mdogo, utafiti huu unaweka pia matarajio ya kuongeza tija.
Utafiti unalenga kupata aina za mbegu za maharage zenye uwezo wa kufikia kati ya tani 1.5 hadi 3 kwa hekta, ikilinganishwa na kiwango cha karibu kilo 900 kwa hekta kinachopatikana katika baadhi ya mazingira ya uzalishaji.
Hata hivyo, haya ni matarajio ya utafiti, si mavuno ambayo tayari yamepatikana kwa wakulima. Uthibitishaji wa kiwango hicho utahitaji majaribio zaidi katika mazingira halisi ya uzalishaji.
BENKI YA VINAASABA KWA KILIMO CHA KESHO
Thamani ya mradi haipo kwenye aina za awali 18 pekee. Kupitia utafiti huo, mtafiti huyo kutoka SUA anasema amekusanya na kuhifadhi aina 130 za maharage ya kienyeji na aina 36 zilizoboreshwa, hatua inayojenga hazina ya vinasaba inayoweza kutumika katika tafiti na uboreshaji wa mbegu siku zijazo.
Mradi pia umehusisha wanafunzi watatu wa shahada ya kwanza waliopata mafunzo ya vitendo kuhusu uchavushaji na uchaguzi wa mimea bora, utambuzi wa vinasaba vya ukinzani wa magonjwa maabara na uhifadhi wa vinasaba hasa kwenye zao la maharage.
Miundombinu ya utafiti nayo imeboreshwa ili kuwezesha uchavishaji na majaribio katika mazingira yanayodhibitiwa.
Kwa maana hiyo, uwekezaji wa Sh. Milioni 70 haujaishia kwenye shughuli za shambani. Umeacha pia maarifa, rasilimali za vinasaba, uwezo wa watafiti na miundombinu ambayo inaweza kutumika katika tafiti zijazo.
COSTECH NA TANZANIA YA 2050
Katika maadhimisho ya miaka 40 ya COSTECH, utafiti huu unaonyesha maana pana ya kuwekeza katika sayansi na teknolojia: si kutafuta suluhisho la tatizo la leo pekee, bali kujenga uwezo wa kutatua changamoto za kesho.
Hili linaendana na msisitizo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kuhusu matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu kuongeza uzalishaji na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Leo, maharage hayo bado hayajafika kwa mkulima. Lakini vinasaba vimekusanywa, aina za awali mpya zimezalishwa, watafiti wamejengewa uwezo na msingi wa majaribio zaidi umewekwa.
Iwapo hatua zinazofuata zitathibitisha ukinzani, mavuno na ubora unaohitajika, utafiti huu unaweza kutoa mbegu zitakazosaidia mkulima kukabiliana na ugonjwa ambao leo unaweza kumpotezea sehemu kubwa ya mavuno.
Hapo ndipo Sh. Milioni 70 zinapovuka kuwa fedha za mradi na kuwa uwekezaji katika maarifa, usalama wa chakula na kilimo cha Tanzania ya 2050.
Maoni 0
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!