Nenda moja kwa moja kwenye maudhui
November 5, 2026
Makala Lucy Ngowi 4

Mgallu: Mwaka Mmoja Wa Samia Wafungua Fursa Mpya Za Maendeleo

Mbunge wa Bagamoyo ataja mafanikio ya amani, uchumi, nishati na madini, asema miradi iliyosubiriwa kwa muda mrefu inaanza kutekelezwa

Na Lucy Ngowi

DODOMA: NDOTO ya muda mrefu ya kuifanya Bagamoyo kuwa kitovu cha viwanda na biashara inaanza kupata uhalisia. Ujenzi wa bandari umeanza kwa hatua za awali, huku viwanda saba kati ya 150 vilivyopangwa katika eneo maalumu la viwanda vikianza kujengwa.

Hayo ni miongoni mwa mafanikio ambayo Mbunge wa Bagamoyo, Subira Mgallu, anayataja kuwa ushahidi wa kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika mwaka mmoja wa awamu ya pili ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu alipoapishwa Novemba 3, 2025.

Mgallu, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, anasema mwaka huo mmoja umeonesha hatua mbalimbali zilizochukuliwa katika kuimarisha amani, kukuza uchumi na kuboresha huduma muhimu kwa wananchi.

Anasema mafanikio hayo yanaonekana katika maeneo mbalimbali, lakini jambo analolipa uzito wa pekee ni kuendelea kuwepo kwa amani na utulivu nchini, ambavyo ni msingi wa shughuli zote za maendeleo.

Habari Picha 14268

Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Subira Mgallu

Kwa mujibu wa Mgallu, Rais Samia alipoingia madarakani alikabiliwa na mazingira yaliyohitaji busara na uongozi makini, hasa kutokana na changamoto zilizojitokeza baada ya uchaguzi.

Anasema kupitia uongozi wake, hali ya kawaida imeendelea kurejea na wananchi wameweza kuendelea na shughuli zao za kila siku.

“Jambo kubwa ambalo nataka kulisema katika mwaka huu mmoja ni namna Mheshimiwa Rais alivyosimamia suala la amani na kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa na utulivu. Bila amani, hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana kwa kiwango kinachotarajiwa,” anasema.

Anabainisha kuwa kufanyika kwa mikutano mbalimbali ya kimataifa nchini na kuongezeka kwa wawekezaji wanaokuja kutafuta fursa ni miongoni mwa ishara zinazoonesha umuhimu wa amani na mazingira mazuri ya uwekezaji.

Akizungumzia uchumi, Mgallu anasema Serikali imeendelea kuongeza uwezo wa kugharamia shughuli za maendeleo kwa kutumia mapato ya ndani, jambo linaloonesha hatua za kuelekea kujitegemea kiuchumi.

Anataja pia kuendelea kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuvuka malengo ya ukusanyaji wa mapato kuwa ishara ya kuendelea kwa shughuli za biashara na uchumi nchini.

Hata hivyo, anasema eneo ambalo amekuwa akilifuatilia kwa karibu ni nishati, kwa kuwa upatikanaji wa umeme na mafuta una mchango mkubwa katika uzalishaji, biashara na ukuaji wa uchumi.

Katika kipindi hicho, anasema Tanzania imeendelea kupata mafuta licha ya changamoto za kimataifa zilizosababishwa na migogoro katika baadhi ya maeneo duniani, ambayo imeathiri usafirishaji na upatikanaji wa bidhaa hiyo.

Anasema Serikali imeendelea kuchukua hatua kuhakikisha mafuta yanapatikana nchini na kupunguza makali ya ongezeko la bei kwa wananchi kupitia hatua mbalimbali za kisera.

Katika nishati ya umeme, anasema hatua muhimu ni kukamilika kwa miundombinu ya kusafirisha umeme kutoka Rufiji kupitia Chalinze hadi Dodoma, iliyogharimu zaidi ya Sh.Bilioni 600.

Anasema miundombinu hiyo ni muhimu kwa sababu uzalishaji wa umeme pekee hautoshi bila kuwa na njia za kuusafirisha kwenda kwa wananchi na maeneo ya uzalishaji.

Pia, Serikali inaendelea na miradi ya kuunganisha mikoa ya Lindi, Mtwara na Rukwa katika gridi ya taifa, pamoja na mradi wa kuunganisha mifumo ya umeme ya Tanzania na Zambia.

Kwa upande wa madini, Mgallu anasema Serikali imeendelea kuwawezesha wachimbaji wadogo ili nao wanufaike na rasilimali zilizopo nchini.

Anataja kukabidhiwa kwa mikopo ya Sh. Bilioni 50 kwa wachimbaji wadogo kupitia Benki ya CRDB kuwa hatua muhimu ya kuwawezesha kupata mitaji na kuongeza uzalishaji.

Anasema juhudi hizo zinaendana na ongezeko la mchango wa sekta ya madini katika mapato ya Serikali, ambapo katika mwaka wa fedha 2025/26 sekta hiyo ilikusanya zaidi ya Sh. Trilioni 1.4 dhidi ya lengo la Sh. Trilioni 1.3.

Aidha, anasema uamuzi wa kutenga asilimia 10 ya fedha zinazotokana na tozo husika kwa ajili ya utafiti wa madini ni hatua nyingine muhimu itakayosaidia kuimarisha sekta hiyo.

Anasema utafiti wa kina utawezesha Serikali kupata taarifa sahihi kuhusu maeneo yenye madini, hivyo kuwasaidia wachimbaji na wawekezaji kufanya maamuzi kwa kutumia taarifa badala ya kutegemea kubahatisha.

Katika eneo la miundombinu, Mgallu anasema Serikali imeendelea kuimarisha barabara kupitia fedha zinazotokana na tozo za mafuta, ambazo zinaelekezwa kwenye mifuko ya matengenezo ya barabara inayosimamiwa na TANROADS na TARURA.

Anasema utaratibu huo unaongeza uhakika wa fedha za kutunza na kukarabati barabara, huku miradi ya maji na elimu ikiendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali.

Kwa upande wa elimu, anasema Serikali imeendelea kupeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule, madarasa, vyoo na miundombinu mingine, ikiwa ni maandalizi ya ongezeko la wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na sekondari katika miaka ijayo.

Hata hivyo, anasema mafanikio hayo yanajidhihirisha zaidi anapozungumzia Bagamoyo, ambako miradi ya muda mrefu inaanza kutekelezwa kwa kasi.

Anasema kwa miaka mingi wananchi wa Bagamoyo wamekuwa na matarajio ya kuona bandari na eneo la viwanda vikijengwa ili kufungua fursa za ajira na biashara.

“Kwa muda mrefu tumekuwa na ndoto ya kuiona Bagamoyo ikiwa na bandari na viwanda. Miradi hii imezungumziwa kwa miaka mingi, lakini sasa tunaona hatua za utekelezaji zikichukuliwa,” anasema.

Anasema ujenzi wa bandari umeanza kwa hatua za awali, ikiwamo ujenzi wa gati la kupokelea mizigo na vifaa vya ujenzi.

Kuhusu eneo la viwanda, anasema mpango ni kujenga viwanda 150, huku saba vikiwa vimeanza kujengwa.

Anasema kukamilika kwa miradi hiyo kutaleta mabadiliko makubwa kwa wananchi kwa kuongeza nafasi za ajira, kukuza biashara na kuongeza mapato ya Serikali.

Pia, anataja miradi ya ujenzi na uboreshaji wa barabara inayounganisha Bagamoyo na maeneo mengine kuwa muhimu katika kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa.

Kwa Mgallu, hatua hizo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi imara, shindani na unaowanufaisha wananchi wengi.

Anasema mwaka mmoja ni mwanzo wa safari ambayo inahitaji ushirikiano wa Serikali na wananchi ili mipango iliyowekwa iweze kutekelezwa na kuleta matokeo yanayoonekana.

Anawataka Watanzania kuendelea kulinda amani, kufanya kazi kwa bidii na kushiriki katika shughuli za maendeleo, akisisitiza kuwa utulivu wa nchi ni msingi wa mafanikio ya sasa na yajayo.

Je, habari hii ilikusaidia?
Sambaza

Maoni 0

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!

Acha maoni

Barua pepe yako haitachapishwa. Sehemu zenye * ni lazima.