Na Lucy Lyatuu,Dodoma
MKUU wa Wilaya ya Dodoma Alhaj Jabir Shekimweri amesema Serikali imeongeza kasi ya maandalizi ya kukabiliana na athari za mvua zinazotarajiwa kunyesha kwa wingi, huku akipongeza Wizara ya Kilimo kwa kuanza ujenzi wa bwawa katika Uwanja wa Maonesho ya Nane Nane kwa ajili ya kuvuna maji ya mvua.
Amesema hatua hiyo imetekelezwa kufuatia maelekezo ya Rais Dkt, Samia Suluhu Hassan, kwa kila mkoa na wilaya kujiandaa mapema dhidi ya athari za mvua, huku akieleza kuwa bwawa hilo linaweza kuwa fursa kwa wananchi kupitia shughuli za umwagiliaji na ufugaji wa samaki.
Amesema hayo baada ya kutembelea uwanja wa maonesho ya nanenane kwa ajili ya kukagua shughuli ya ujenzi wa bwawa hilo pamoja na kuona ujenzi wa mitaro na barabara katika eneo hilo.

Amesema pamoja na hatua zinazochukuliwa katika maeneo ya katikati ya jiji, maandalizi yanapaswa kuimarishwa pia katika maeneo ya pembezoni, ikiwemo Mbolo, Gawaye, Nzinge, Zuzu, Babala, Mkulabi na Mpunguzi, ambayo yamewahi kuathiriwa na mvua na kusababisha baadhi ya barabara kutopitika.
Aidha, amezitaka taasisi zinazohusika na ujenzi na uchimbaji wa vifaa vya ujenzi kuhakikisha maeneo wanayofanyia shughuli hizo yanarejeshwa katika hali salama kwa kuzingatia mipango ya usimamizi wa mazingira, huku akiwataka wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi ya mafuriko kuanza kuchukua hatua mapema, ikiwemo kuhamisha mali na familia zao kwenda maeneo salama.

Kwa upande wake,Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Dkt Frederick Sagamiko amesema jiji hilo limeunda kamati ya wataalamu kwa ajili ya kuratibu hatua za kukabiliana na changamoto ya mafuriko, huku ikishirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali, TARURA na Shirika la Msalaba Mwekundu.
Amesema Halmashauri hiyo inaendelea kusafisha na kuzibua mifereji ya maji, huku ikieleza kuwa mipango miji isiyozingatiwa, ikiwemo ujenzi katika korongo na kuziba njia za maji, ni miongoni mwa mambo yanayoweza kuongeza hatari ya mafuriko hata wakati wa mvua za kawaida.
Ameaataka wananchi kuondoa kwa hiari baadhi ya miundombinu iliyojengwa kwenye mitaro na mifereji ya maji, pamoja na kutoa taarifa kwa Halmashauri kupitia watendaji wa maeneo yao pale wanapoona njia za maji zimezibwa.

“Halmashauri inaendelea kuimarisha usafi wa mazingira na mifereji kwa kushirikiana na TARURA, huku ikisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wananchi na taasisi mbalimbali katika kukabiliana na athari za mafuriko”, amesema.
Mkandarasi wa mradi wa ujenzi wa barabara unaohusisha udhibiti wa maji katika eneo la NZuguni, Bazili Amas kutoka kampuni ya Expediture Limited (EMC), amesema utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 75.
Amesema hadi sasa wamekamilisha ujenzi wa barabara pamoja na mifereji inayosafirisha maji kwenda kwenye bwawa, hatua inayolenga kupunguza maji yanayoelekea kwenye makazi ya wananchi.
Aidha, amesema wamejenga matuta katika maeneo ambayo barabara zinavuka, ili kuzuia maji kuvuka na kuelekea kwenye makazi ya wananchi.
Bazili amesema kazi hiyo ilianza Machi 2026 na inatarajiwa kukamilika Februari 2027, huku akiahidi kuwa mkandarasi atahakikisha mradi unakamilika kwa wakati.



Maoni 0
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!