Na Lucy Lyatuu,Dodoma
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amezindua Sera ya Maendeleo Ya Viwanda ya mwaka 2025 na kuzitaka taasisi za umma kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini katika ujenzi, ununuzi wa samani na mahitaji mengine, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kukuza viwanda, kulinda ajira na kuongeza mapato ya Taifa.
Ametoa maelekezo hayo, wakati akimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uzinduzi wa Sera hiyo na Sera ya Maendeleo ya Jasiriamali Ndogo na za Kati ya Mwaka 2003 (Toleo la Mwaka 2025), katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete, Dodoma.
Amesema dhana ya kununua bidhaa za ndani ianzie serikalini kwa kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini.

Dkt. Mwigulu ametaja vioo, nondo, marumaru na samani kuwa miongoni mwa bidhaa zinazozalishwa nchini ambazo taasisi za umma zinapaswa kutumia, akisisitiza kuwa Serikali lazima iongoze kwa vitendo katika kutekeleza sera inazozitunga.
“Tumeweka sera, kwa hiyo lazima tuyaishi maneno yetu,” amesema akitaka sheria ziangaliwe na kurekebishwa iwapo zina mianya inayokwamisha matumizi ya bidhaa za ndani au kutoa nafasi ya kukwepa utekelezaji wa maelekezo hayo.
Amesema jitihada za kujenga viwanda haziwezi kuleta matokeo yaliyokusudiwa ikiwa bidhaa zinazozalishwa hazitumiki, kwa kuwa kukosekana kwa soko kunapunguza uzalishaji, ajira na mapato.
“Tutumie bidhaa zinazozalishwa nchini kwa kujiamini, kufurahia na kujivunia, ili kulinda viwanda vyetu, ajira na mapato ya nchi yetu, pamoja na kukuza uchumi,” amesema.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amewataka watendaji wa Serikali kubadili mtazamo kuhusu sekta binafsi na kuitambua kuwa mshirika muhimu katika kujenga uchumi unaojitegemea.
Amesisitiza umuhimu wa kuheshimu mitaji na uwekezaji, pamoja na kuendeleza mazingira yanayoiwezesha sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi.
Kuhusu utekelezaji wa sera zilizozinduliwa, Dkt. Mwigulu ameielekeza Wizara ya Viwanda na Biashara kuandaa mikakati thabiti, kufanya ufuatiliaji na tathmini, pamoja na kushirikiana na wizara za kisekta na sekta binafsi kuhakikisha malengo yanafikiwa.
Pia, ameitaka wizara kusimamia na kuratibu minyororo ya thamani ili kuwezesha jasiriamali ndogo na za kati kuzalisha malighafi na kutoa huduma zinazohitajika viwandani.

Amesema Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji, pamoja na kuboresha miundombinu ya nishati, maji, barabara na reli ili kuongeza uwezo wa viwanda kushindana katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema wizara imeandaa mkakati wa utekelezaji wa miaka 10 wenye shabaha za kila mwaka, ambazo zitafuatiliwa na kutathminiwa ili kuhakikisha sera hizo zinaleta matokeo.
Amesema utekelezaji huo utawapa nafasi jasiriamali ndogo na za kati na kupanua masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini, hususan katika masoko ya kikanda na Afrika.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema sera hizo zinaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na ni nyenzo muhimu za utekelezaji wake.


Maoni 0
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!