Nenda moja kwa moja kwenye maudhui
November 6, 2026
Habari Author 3

Program Ya Ushirikiano Wa Maendeleo Ya Viwanda Yazinduliwa

Na Lucy Lyatuu,Dodoma
NAIBU  Waziri wa Viwanda na Biashara, Denis Londo, amesema Tanzania haina budi kuachana na uchumi wa kuuza malighafi nje na badala yake kujikita katika kuongeza thamani ya rasilimali zake kama njia pekee ya kufikia uchumi wa Dola Trilioni moja ifikapo mwaka 2050.
Londo amesema hayo wakati akifungua Kongamano la Maendeleo ya Viwanda na kuzindua rasmi Programu ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Viwanda (PCP) kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) kwa kipindi cha 2026 hadi 2031.
Habari Picha 14288
” Kila kizazi kina jukumu lake la kihistoria, kinapaswa kugundua jukumu hilo, na aidha kulisaliti au kulitekeleza,” alisema Londona kuongeza kuwa Tanzania ina bahati ya kuandika Dira ya 2050 na wakati huo huo kushiriki katika kuitekeleza.
Amesema nadharia ya soko huria duniani inabomoka, ambapo mataifa makubwa sasa yanatumia ushuru na rasilimali kama maji na madini kama silaha za kisiasa na kiuchumi.
“Zamani ushuru ulitumika kulinda viwanda vya ndani, sasa unatumika kama silaha ya kuzuia wengine wasifike walipofika wengine. Maji sasa si usalama au uvuvi tu, maji ni silaha,” amesema, akieleza kuwa ndio maana bei za bidhaa duniani zinapanda na kuathiri hata Watanzania.
Amesema ndio maana umuhimu wa Muungano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar unazidi kuwa mkubwa katika kutumia uchumi wa buluu  kama nguzo ya viwanda.
Habari Picha 14289
Kuhusu  PCP iliyozinduliwa  amesema  inaakisi moja kwa moja Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo msingi wake mkuu ni mageuzi ya vijijini.
“Hatuzungumzii kuongeza idadi ya viwanda tu, tunazungumzia kuzalisha tija, ajira na ustawi wa wananchi vijijini ambako Watanzania wengi wanaishi,” amesisitiza.
Londo amesema kuwa Sheria ya Fedha ya mwaka 2026/2027 imeelekeza asilimia tano ya mapato yote ya ndani ya halmashauri nchini kuelekezwa kujenga miundombinu ya uzalishaji ikiwemo maeneo ya uwekezaji na kongani za viwanda, pamoja na asilimia 10 ya awali kwa makundi ya wanawake, vijana na walemavu na Wizara kupitia SIDO na TAMISEMI itahakikisha fedha hizo zinawafikia walengwa.
Aidha, amekumbusha kuwa utekelezaji wa Dira ya 2050 unategemea asilimia 70 ya nguvu ya sekta binafsi, na kwamba ni mujimu kujifunza kutokana na makosa ya ubinafsishaji wa viwanda vya zamani.
“Tunajua tulipokosea tulipobinafsisha viwanda vyetu. Kongamano hili lijadili ni aina gani ya sekta binafsi tunayoitaka ishiriki kutimiza Dira ya 2050,” amesema.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Balozi Waziri Salum, amesema kongamano hilo limeandaliwa mahususi kujadili fursa, changamoto na hatua za kuongeza uwekezaji, uzalishaji na uongezaji thamani ya malighafi za ndani.
Habari Picha 14290
Amesema   kupitia PCP, Serikali inatarajia kuimarisha uratibu wa miradi ya viwanda, kukuza ujuzi, kuvutia uwekezaji, kuongeza mauzo ya nje na kuendeleza uzalishaji unaozingatia utunzaji wa mazingira , Programu hiyo itatekelezwa kwa pamoja Tanzania Bara na Zanzibar kwa kuunganisha rasilimali, teknolojia na uwekezaji kutoka kwa wadau mbalimbali.
Amesema Wizara itahakikisha maoni na mapendekezo yote yatakayotolewa na wadau katika kongamano hilo yanafanyiwa kazi kwa kushirikiana na taasisi husika ili kuhakikisha kongamano linaleta matokeo ya kweli kwa maendeleo ya viwanda nchini.
Je, habari hii ilikusaidia?
Sambaza

Maoni 0

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!

Acha maoni

Barua pepe yako haitachapishwa. Sehemu zenye * ni lazima.