Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Kuendeleza na Kuhamisha Teknolojia ndani ya COSTECH, Dkt. Erasto Mlyuka, akiwa na David Denis, mmoja wa vijana 15 walioingizwa katika mpango maalumu wa kuwawezesha wabunifu kulinda bunifu zao kupitia hataza.
Na Lucy Ngowi
KILA siku, nywele hukatwa kwenye saluni na mara nyingi huishia kwenye mifuko ya taka. Kwa wengi ni uchafu unaopaswa kuondolewa. Kwa David Denis, mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa CutOff Recycle Limited, ni malighafi yenye thamani.
Kutokana na taka hizo, Denis ameunda teknolojia inayozibadilisha kuwa bidhaa za kilimo, zikiwemo mbolea ya kimiminika yenye amino asidi, mbolea hai na virutubisho vya mimea.
Hivyo, taka ya saluni inabadilika kutoka uchafu kuwa malighafi, malighafi kuwa teknolojia, teknolojia kuwa bidhaa na bidhaa kuwa fursa kwa mkulima.
Safari hiyo sasa imevuka hatua ya wazo na majaribio na kuingia katika eneo la hataza, uzalishaji, watumiaji na soko. Inatoa pia picha ya namna Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) inavyoweza kusaidia wazo la Mtanzania kulindwa kwa haki miliki na kuelekea kwenye thamani ya kiuchumi.

Kwa mujibu wa Denis, safari yake ilianza mwaka 2018 kama mradi wa shule baada ya kutambua changamoto ya utupaji wa taka za nywele na uwezekano wa kuzitumia kama rasilimali katika kilimo.
Leo, CutOff Recycle hukusanya taka za nywele kutoka saluni na kuzibadilisha kuwa bidhaa zinazolenga kuboresha afya ya udongo na uzalishaji wa mazao.
Hata hivyo, kutoka wazo hadi biashara kulihitaji utafiti, majaribio, teknolojia, ulinzi wa haki miliki, bidhaa inayoweza kutumiwa na mkulima na mfumo wa kibiashara.
Hapo ndipo safari ya Denis inapokutana na COSTECH.
COSTECH: Daraja kutoka ubunifu hadi umiliki
Oktoba mwaka huu, COSTECH inaadhimisha miaka 40 ya uongozi katika sayansi, teknolojia, ubunifu na uratibu wa utafiti nchini.
Katika miaka ya karibuni, tume hiyo imeunga mkono wabunifu 125, kufadhili miradi 57 ya utafiti kati ya 2021 na 2025 na kuvutia zaidi ya Sh. Bilioni 60 kutoka Serikali na washirika wa maendeleo, huku ikiendelea kujenga mifumo ya kusaidia ubunifu kufikia hatua ya kibiashara.
Kwa Denis, hatua muhimu ilikuja mwaka 2023 aliposhiriki Mpango wa Kitaifa wa Mafunzo kwa Wabunifu Vijana, uliofanyika Dodoma na kulenga kuimarisha ubunifu, uundaji wa bidhaa na umiliki wa haki miliki.

Program ya Kitaifa ya Mafunzo kwa Vijana Wabunifu Tanzania – Awamu ya Kwanza iliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia ambayo David Denis alikuwa miongoni mwa washiriki
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Kuendeleza na Kuhamisha Teknolojia ndani ya COSTECH, Dkt. Erasto Mlyuka, Denis alikuwa miongoni mwa vijana 15 walioingizwa katika mpango maalumu wa kuwawezesha wabunifu kulinda bunifu zao kupitia hataza.
Msaada huo ulihusisha uandishi na uandaaji wa nyaraka za haki miliki, hatua iliyosaidia kuimarisha njia kutoka ubunifu hadi umiliki wa teknolojia.
Hatua hiyo ilizaa matokeo. Hataza yenye namba TZ/P/2024/00036 ilitolewa Septemba 18, 2024 kwa uvumbuzi unaohusu njia ya kutengeneza mbolea ya kimiminika yenye amino asidi kutokana na taka za nywele za binadamu.
Kwa Denis, hataza hiyo ni msingi wa kisheria wa kulinda teknolojia na kufungua nafasi ya uzalishaji, uwekezaji, ushirikiano na upanuzi wa soko.
Kampuni imejenga pia chapa za bidhaa zake, zikiwemo Rutubisha, McheKuza na Vuna, huku ikiendelea kuendeleza bidhaa zinazotokana na taka za nywele.
Mwaka 2026, kampuni imewasilisha ombi la kimataifa lenye namba PCT/IB2026/050342 kwa teknolojia ya mfumo wa kusambaza mbolea unaotumia akili bandia, unaolenga kuboresha upatikanaji wa mbolea Tanzania na nje ya nchi.
Hivyo, safari haijaishia kwenye hataza moja, bali inaendelea kuelekea kujenga jalada la teknolojia, bidhaa na haki miliki.
Dalili nyingine kwamba teknolojia imevuka hatua ya majaribio ni uwezo wa uzalishaji.
Denis anaeleza kuwa kampuni imefikia uzalishaji wa takribani tani tano za mbolea ya kupandia kwa wiki, sawa na karibu tani 20 kwa mwezi, huku ikilenga kuongeza uwezo huo.

Kampuni pia iko katika hatua za kuendeleza uzalishaji wa mbolea za maji kupitia eneo la SIDO Arusha, ambalo limetoa ardhi kusaidia upanuzi wa uzalishaji.
“Mahitaji bado yanatuzidi. Tunahitaji kuongeza uzalishaji ili tuweze kukidhi mahitaji ya soko,” anasema Denis.
Kauli hiyo inaonyesha changamoto mpya: si tena kuthibitisha kama teknolojia inawezekana, bali kuizalisha kwa kiwango kikubwa na kukidhi mahitaji.
Kampuni hukusanya malighafi kupitia vituo vilivyopo Dar es Salaam, Kilimanjaro na Arusha, huku ikilenga kupanua mtandao huo.
Sh300 kwa kilo: taka inakuwa kipato
Katika mfumo huo, mtu anayekusanya taka si kiungo cha pembeni. CutOff Recycle inaeleza kuwa wakusanyaji hulipwa Sh300 kwa kila kilo ya taka za nywele wanayopeleka kwenye vituo vyake.
Hivyo, saluni inakuwa chanzo cha malighafi, mkusanyaji anapata kipato, kampuni inapata malighafi na mkulima anapata pembejeo.
Kampuni pia ina mkataba wa makubaliano wa ukusanyaji wa taka za nywele za binadamu jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, changamoto ipo kwenye ubora wa taka zinazokusanywa. Denis anasema taka zinapochanganywa na vitu visivyohitajika, hutengeneza ugumu wa kuzitenganisha na kuchakata.
Zaidi ya watumiaji 100: bidhaa imefika kwa mkulima
Mwisho wa teknolojia si maonesho wala hataza; ni mtumiaji.
Kwa sasa, kampuni inaeleza kuwa bidhaa zake zimefikia watumiaji zaidi ya 100, ishara kwamba teknolojia hiyo imeanza kuingia katika matumizi.
Mpemba, mkulima wa mahindi kutoka Mbeya, anasema alipotumia mbolea ya kampuni hiyo, mimea ilikua ikiwa na kijani na afya zaidi na aliripoti ongezeko la mavuno la karibu asilimia 40 ikilinganishwa na msimu uliopita.
Happyness Makundi, mkulima wa maua kutoka Arusha, anasema kutumia virutubisho vya kampuni hiyo kulimsaidia kupunguza matumizi ya maji na muda wa maandalizi.
Kwa Nashe, mkulima wa nyanya kutoka Arusha, thamani nyingine ni ushauri wa shamba anaoupata kabla na baada ya kununua bidhaa.
Ushuhuda huu si majaribio huru ya kisayansi, lakini unaonyesha bidhaa imeanza kuwafikia watumiaji na kupata uzoefu wa matumizi shambani.
Kutoka taka hadi bidhaa za kilimo
Miongoni mwa bidhaa hizo ni Amino Acid+ Crop Booster, mbolea ya kimiminika inayotokana na nywele zilizorejelewa na yenye nitrojeni na amino asidi.
Kuna pia McheKuza, bio-mbolea inayolenga kuchochea ukuaji wa awali wa mimea na kuboresha afya ya udongo, pamoja na Nutrified Growing Medium, inayolenga kuboresha muundo wa udongo na uwezo wa kuhifadhi maji.
Hivyo, teknolojia haijaishia kwenye bidhaa moja, bali imeanza kujengwa kuwa mfumo wa bidhaa za kilimo unaotokana na taka za nywele.
Kutoka Tanzania hadi soko la dunia
Hatua nyingine ya ukuaji ni kutafuta masoko nje ya Tanzania. Kampuni imeingia katika ushirikiano na Alibaba.com kwa ajili ya kufikia masoko ya kimataifa.
Kwa maana hiyo, teknolojia ya ndani haipaswi kuishia kutatua tatizo la ndani pekee; ikiwa bidhaa ina uwezo wa kushindana, inaweza kuingia katika masoko mapana.
Mafanikio yaliyomweka kwenye ramani
Kwa mujibu wa kampuni, mwaka 2020 Denis alichaguliwa kuwa miongoni mwa wajasiriamali vijana bora wa Afrika kupitia Anzisha Prize; mwaka 2021 alishika nafasi ya pili duniani katika Global Student Entrepreneur Awards; mwaka 2022 aliingia 15 bora katika Startupper of the Year; mwaka 2023 alikuwa nusu fainali wa Extreme Tech Challenge; na mwaka 2025 alishinda mashindano ya ubunifu ya Innovation Week Arusha.
Mafanikio hayo yanaonyesha safari iliyoendelea kupitia mafunzo, mashindano, ulinzi wa haki miliki, bidhaa, biashara na watumiaji.

TFRA: Ubunifu lazima ufuate sheria
Katika Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu, Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Gothard Liampawe, anasema jukumu la mamlaka hiyo si kuzuia ubunifu, bali kuhakikisha bidhaa zinazofika kwa wakulima zinakidhi matakwa ya ubora na sheria.
“Watu wanafikiri sisi kama mamlaka tunadhibiti mbolea zinazotoka viwandani tu, lakini tunadhibiti pia mbolea za asili,” anasema.
Kwa Liampawe, ubunifu wa mbolea lazima uambatane na taratibu za usajili, ubora na usalama ili bidhaa iingie sokoni kwa uhalali.
Hapo ndipo mfumo wa ubunifu unavyoungana: COSTECH inawezesha ubunifu, haki miliki inalinda umiliki, TFRA inasimamia udhibiti, uzalishaji unaongeza thamani na soko linatoa kipimo cha mwisho.

Baada ya hataza: changamoto ni kukua
Kwa Denis, changamoto kubwa kwa wabunifu wengi nchini si ukosefu wa mawazo, bali uwezo wa kuyageuza kuwa biashara zinazoweza kukua.
Anataja mahitaji ya mtaji, mashine, maeneo ya uzalishaji na miundombinu. Kwa baadhi ya wazalishaji vijana, anasema mahitaji yanaweza kufikia Sh. milioni 300 hadi 400 ili kuanzisha au kupanua uzalishaji.
“Unaweza kupewa fedha za kununua malighafi, lakini kama huna sehemu ya kuwekeza, sehemu ya kuchakata na mashine za uzalishaji, inakuwa ngumu,” anasema.
Anashauri Serikali kuimarisha kongani za viwanda na maeneo maalumu ya uzalishaji yatakayowapa wabunifu mazingira ya kuzalisha kwa gharama nafuu.
Hoja hiyo inaendana na mwelekeo wa COSTECH wa kusaidia ubunifu kufikia hatua ya kibiashara, ikiwemo programu zinazolenga kusaidia bidhaa za wabunifu kufikia hatua ya kuthibitishwa na kuuzwa pamoja na mpango wa dhamana ya mikopo kwa biashara bunifu zilizo tayari kuingia sokoni.
COSTECH: Wazo moja, somo kwa taifa
Miaka 40 ya COSTECH ina maana zaidi pale inapoweza kuonyesha matokeo yanayoonekana katika maisha ya wabunifu.
Safari ya Denis inaonyesha mlolongo ambao ubunifu unapaswa kupitia: wazo, utafiti, majaribio, teknolojia, haki miliki, bidhaa, mtumiaji, soko, uwekezaji, uzalishaji mkubwa na ukuaji endelevu.
Hapo ndipo kaulimbiu “Kutoka Taka hadi Utajiri: Ubunifu kwa Dira ya 2050” inapopata maana.
Dira ya Tanzania ya 2050 inahitaji uchumi unaotumia maarifa, teknolojia, ubunifu na kuongeza thamani ya rasilimali zilizopo nchini.
Katika muktadha huo, taka za nywele zinaweza kuonekana kama kitu kidogo. Lakini zikichanganywa na sayansi, teknolojia, haki miliki na ujasiriamali, zinaweza kuwa sehemu ya mnyororo wa thamani unaozalisha bidhaa, kipato na fursa za ajira.
Mwisho wa safari hii hauko saluni ambako nywele hukatwa, bali shambani ambako bidhaa hiyo inatumika.
Nywele iliyofagiliwa inaweza kuwa malighafi. Malighafi inaweza kuwa teknolojia. Teknolojia inaweza kulindwa kwa hataza. Hataza inaweza kuwa msingi wa uwekezaji. Uwekezaji unaweza kuongeza uzalishaji na uzalishaji unaweza kumfikia mkulima.
Hapo ndipo taka inapogeuka kuwa dhahabu ya kijani.
Kwa CutOff Recycle, kazi kubwa sasa si kuthibitisha kwamba taka zinaweza kutumika. Tayari imeanza kugeuza taka kuwa bidhaa na kuwafikia watumiaji.
Hatua inayofuata ni kukusanya zaidi, kuzalisha zaidi, kuwafikia wakulima wengi zaidi, kuimarisha ushahidi wa matumizi, kupanua soko na kuifanya teknolojia ya Tanzania ishindane katika masoko mapana.
Na kwa COSTECH, baada ya miaka 40 ya kujenga mazingira ya sayansi, teknolojia na ubunifu, changamoto ya kizazi kijacho ni kuhakikisha visa kama vya David Denis havibaki kuwa hadithi za mafanikio ya mtu mmoja, bali vigeuke kuwa biashara zinazokua, teknolojia zinazolindwa, ajira zinazozalishwa, mazingira yanayolindwa na suluhisho za Tanzania zinazoweza kwenda duniani.



