Na Lucy Ngowi
DODOMA: WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) umeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma zake mbalimbali na miradi ya uwekezaji inayotekelezwa nchini kupitia ushiriki wake katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea jijini Dodoma.
Akizungumza katika maonesho hayo, Meneja wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa TBA, Lumuli Mwangosi, amesema taasisi hiyo inatumia fursa hiyo kuwafahamisha wananchi kuhusu majukumu yake pamoja na huduma zinazotolewa kwa lengo la kuboresha ustawi wa jamii na maendeleo ya taifa.
Amesema TBA hutoa huduma za ushauri wa ujenzi wa majengo ya serikali, upangishaji wa nyumba za watumishi wa umma na ofisi, pamoja na kushiriki katika utekelezaji wa miradi ya uwekezaji kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Kwa mujibu wa Mwangosi, wakala huo unaendelea kutekeleza miradi mbalimbali katika mikoa tofauti ikiwemo Dar es Salaam, Mwanza na Arusha, huku ukitumia maonesho hayo kuwaelimisha wananchi kuhusu fursa zinazopatikana kupitia miradi hiyo.
“Wananchi wanaotembelea banda letu wanapata nafasi ya kufahamu huduma tunazotoa, kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali na kujionea hatua za miradi inayotekelezwa na TBA,” amesema.
Ameeleza kuwa kaulimbiu ya mwaka huu ya ‘Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu’ inaakisi dhamira ya taasisi hiyo ya kuhakikisha watumishi wake wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi, uwazi na uwajibikaji ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Aidha, amesema TBA imeendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia za kidijitali katika shughuli zake za kila siku ili kuongeza ufanisi na kurahisisha utendaji kazi.
Baadhi ya mifumo inayotumika ni pamoja na Watumishi Portal, Mrejesho, Msawazo, mifumo ya mikopo pamoja na mfumo wa usimamizi wa utendaji kazi wa PePMIS.
Mwangosi ameongeza kuwa taasisi hiyo inaendelea kuwekeza katika maendeleo ya rasilimali watu kupitia mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu yanayolenga kuongeza ujuzi wa watumishi na kuwawezesha kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia pamoja na mahitaji ya kisasa ya utoaji huduma.
Amesema mafunzo hayo yanawahusisha watumishi wa kada mbalimbali, wakiwemo wahandisi na watumishi wa utawala, kwa lengo la kuimarisha utendaji kazi na kuongeza tija katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi.

