Na Mwandishi Wetu
SERIKALI inaendelea na juhudi za kupunguza mzigo wa tozo kwa Wachimbaji wadogo wa dhahabu hapa nchini kwa kufanya mapitio ya ada na ushuru mbalimbali anazotozwa katika mnyororo wa uchimbaji na uchenjuaji wa madini.
Waziri wa Madini Anthony Mavunde, amesema hayo Bungeni Jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Busanda, Tumaini Magessa ambaye alitaka kujua ni lini Serikali itapitia upya tozo zilizopo kwenye mnyororo wa uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu zinazowaelemea Wachimbaji Wadogo.
Katika majibu yake, Waziri Mavunde amesema kuwa kupitia Mkakati wa Kuboresha Mazingira ya Biashara, Wizara ya Madini imefanya utafiti wa tozo 66 zinazotozwa na Halmashauri mbalimbali katika shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu.
Ametaja tozo hizo kuwa ni ushuru wa karasha, ada ya ukaguzi, kodi ya thamani, ushuru wa kusafirisha miamba ya madini, na visusi (mabaki ya miamba baada ya uchenjuaji).
“Katika kutatua changamoto hizi, Wizara iliitisha kikao Mwezi Agosti, 2024 Mkoani Singida ambacho kilishirikisha Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Wizara ya Fedha, Tume ya Madini, STAMICO, Halmashauri za Wilaya (Ikungi, Chunya, Kahama, Msalala, Meatu, Shinyanga, Mtama na Lindi),
“FEMATA na TAWOMA. Rasimu ya Mapendekezo ya Maboresho tayari imeshaandaliwa na ipo katika hatua ya kufanyiwa mapitio na tathmini, ambapo Matokeo ya tathmini hiyo yatatusaidia katika kupanga tozo rafiki kwa wachimbaji wadogo,” amesema.
Pia amesema serikali inaendelea na maboresho makubwa ya mfumo wa kodi kupitia Tume ya Maboresho ya Kodi iliyoanzishwa na Rais Samia Suluhu Hassan, tume hiyo inatarajiwa kutoa mapendekezo yatakayosaidia kupunguza changamoto za kikodi zinazowakabili wachimbaji hao wadogo.
Hatua hizo zinadhihirisha dhamira ya Serikali katika kuboresha mazingira ya uchimbaji mdogo wa madini na kukuza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa nchi.