MAMLAKA Ya Elimu Na Ufundi Stad Nchini (VETA) imesema inashiriki katika tamasha la nne la kitaifa la utamaduni ili kuonesha mavazi ya utamaduni,bidhaa za utamaduni pamoja na ngoma zinazofundishwa katika vyuo hivyo.
Ofisa Mkuza Mitaala Kutoka VETA, Atanasia Kisieri amesema hayo wakati akizungumza katika banda la VETA lililopo katika Tamasha hilo linaloendelea katika mkoa wa Morogoro.
Amesema katika tamasha hilo kanda moja imeshiriki ikionesha maeneo makuu manne ambayo ni pamona na eneo la mavazi ya utamaduni,mavazi ya asili ya mswahili ambayo wametumia kwa kujifunga kanga kuashiria utamaduni wa watanzania.
“Utamaduni huo ni wa kufunga kanga wakati wa kuoga, wakati wa ujauzito,kumfunika mtoto na hata kutengeneza kata ya kubebea mtungi wa maji na kujifunga kiunoni wakati mabinti wakicheza,”amesema.
Ameongeza kuwa kupitia vyuo vya VETA vya Dakawa,Kihonda,Mikumi na Pwani aameweza kutumia tamasha hilo kuonesha mavazi yanayoakisi utamaduni wa Watanzania ambapo walishona mavazi ya kanga yakichanganywa na kaniki.
Amesema katika vyuo vyote vinne vya VETA vimetumia tamasha hilo kuonesha umahiri mkubwa wa mavazi waliyotengeneza kwa mitindo ya kawaida ikiwemo magauni na kofia pamona na kanga zenye jumbe mbalimbali walizojifunga katika usiku wa Mtanzania katika tamasha hilo.
Kisieri amesema kwa kutumia tamasha hilo wameendelea kudumisha utamaduni wa watanzania ambao ndio urithi ambapo wamesherehesha tamasha lakini pia kutoa mafunzo ya kutengeneza mavazi au bidhaa zinazoendana na utamaduni wa kitanzania.
Amesema VETA imejipanga kurudi kwenye utamaduni kupitia mavazi na kuahidi kutoa mafunzo yenye ubora kwa sekta zote 13 ili kila mmoja kuweza kunufaika na kukuza ujuzi.