Na Lucy Lyatuu,Morogoro
TAASISI ya Chakula na Lishe (TFNC) imewashauri wataalam wa lishe na afya wanaotoa ushauri wa lishe kupitia mitandao ya kijamii kushirikiana na Taasisi zenye mamlaka ili kuhakikisha jamii inapata elimu sahihi yenye ushahidi wa kitaalamu.
Ofisa Lishe Na Mtafiti wa TFNC, Maria Ngilisho amesema hayo katika Tamasha la Nne la Taifa la Utamaduni mkoani Morogoro na kuongeza kuwa taasisi hiyo imepewa dhamana ya kuratibu shughuli za chakula na lishe, ikiwemo kufanya tafiti, kutoa elimu na kujenga uwezo kwa wadau mbalimbali.
Amesema ni kweli wapo wanaotoa huduma za lishe kwa jamii kupitia mitandao ya kijamii na Taasisi imekuwa ikiona hibyo inawahimiza kushirikiana nao ili kufikisha kile kinachotakiwa kwa jamii.

Hata hivyo imesisitiza umuhimu wa jamii kuzingatia ulaji bora na mtindo wa maisha unaofaa katika kudhibiti na kutokomeza aina mbalimbali za utapiamlo nchini.
Amesema kaulimbiu ya taasisi hiyo katika tamasha hilo ni “Chakula Chetu, Utamaduni Wetu, Afya Yetu,” akisisitiza wananchi kula mlo kamili unaojumuisha vyakula kutoka katika makundi sita ili kupata virutubishi muhimu kwa afya.
Ngilisho amesema elimu hiyo inaambatana na umuhimu wa kuzingatia usafi wa mazingira, maji na chakula, kuepuka matumizi ya vileo, sigara na tumbaku, pamoja na kufanya mazoezi kwa angalau dakika 30 kila siku.

Kadhalika ameeleza kuwa maabara ya Taasisi ya Chakula na Lishe huchunguza sampuli za vyakula na binadamu ili kubaini virutubishi na upungufu wa vitamini au madini, huku matokeo yakitumika kutoa ushauri wa kitaalamu kwa Serikali kuhusu hatua za kukabiliana na changamoto za lishe.


