Na Lucy Ngowi
DODOMA: MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imewataka wakulima kutumia viuatilifu vilivyosajiliwa kwa kufuata ushauri wa wataalamu, huku wafanyabiashara na wasafirishaji wakitakiwa kuhakikisha mazao yanakidhi viwango ili kuongeza ushindani wa Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Mamlaka kwa mwaka wa fedha 2025/2026 na mwelekeo wa mwaka 2026/2027.
Profesa Ndunguru amesema wakulima wanapaswa kutoa taarifa mapema wanapoona wadudu au dalili zisizo za kawaida kwenye mazao, kushirikiana na Maofisa Ugani pamoja na wataalamu wa TPHPA na kuepuka matumizi holela ya viuatilifu, ambayo yanaweza kuhatarisha afya ya binadamu, mazingira na masoko.

Kwa wafanyabiashara na wasafirishaji, amesema ni muhimu kuzingatia taratibu za afya ya mimea na kuhakikisha mazao yanakidhi masharti ya nchi wanazokusudia kuuza, hatua itakayosaidia kupunguza changamoto ya mizigo kukataliwa katika masoko ya nje.
Aidha, TPHPA imesema inalenga kuongeza fursa za biashara ya viazi mviringo katika soko la Zambia kwa kusimika mtambo wa kusafishia viazi katika eneo la Makambako.
Hatua hiyo inalenga kuongeza ubora na ushindani wa zao hilo katika masoko ya nje.
Profesa Ndunguru amesema kilimo si uzalishaji pekee, bali ni fursa ya biashara na ajira, hususan kwa vijana, kupitia masoko yaliyofunguliwa na matumizi ya teknolojia za kisasa.

Katika mwaka wa fedha 2025/2026, Tanzania imefikia utoshelevu wa chakula wa asilimia 130, huku uzalishaji ukifikia tani 23,783,128.
TPHPA pia imedhibiti kwelea kwelea milioni 233.5 katika wilaya 21, hatua iliyosaidia kuokoa takribani tani 1,092,780 za nafaka, huku udhibiti wa viwavi jeshi katika Halmashauri 52 ukiokoa takribani tani 342,787.5 za mazao.





