Na Lucy Ngowi, Mwanza
KATIBU Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria yenye makao yake Kisumu, Kenya, Dkt. Masinde Bwire, amesema bila kuchukua hatua muhimu za kisera, kisayansi na kiutendaji, Ziwa Victoria litaendelea kuharibika na kushindwa kuchangia ukuaji wa uchumi, maendeleo ya jamii pamoja na uhifadhi wa ikolojia.
Dkt. Bwire amesema Jumuiya ya Afrika Mashariki ilianzisha maadhimisho ya Siku ya Ziwa Victoria kwa lengo la kuwahamasisha wananchi kulienzi, kulitunza na kulihifadhi ziwa hilo ambalo ni muhimu kwa maisha na uchumi wa watu wa ukanda huo.
Amesema Ziwa Victoria linakabiliwa na shinikizo kubwa la uchafuzi wa mazingira pamoja na matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali zake.
Ameeleza kuwa ukanda wa ziwa umebarikiwa kuwa na madini ya dhahabu, ardhi yenye rutuba inayofaa kwa kilimo na mazao ya viwandani, pamoja na mbuga na hifadhi kubwa kama Serengeti na Maasai Mara ambazo ni muhimu kwa uchumi wa nchi za Afrika Mashariki.
Aidha, amesema ziwa hilo linaunganisha nchi za Tanzania, Kenya na Uganda, hivyo kuwa kiungo muhimu cha biashara, usafirishaji na shughuli nyingine za kiuchumi, jambo linalofanya uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali zake kuwa wa lazima.
Kwa mujibu wa Dkt. Bwire, tafiti zilizofanywa na Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria zimebaini kuwepo kwa kiwango kikubwa cha uchafuzi wa maji katika maeneo mengi ya ziwa na fukwe zake.
Tafiti hizo zimeonyesha uwepo wa kemikali hatarishi ikiwemo zebaki (mercury), taka ngumu, plastiki pamoja na maji taka yanayotiririka kutoka majumbani na viwandani.
Ametaja baadhi ya maeneo yaliyoathirika zaidi kuwa ni Mwanza, Geita, Musoma, Entebbe, Jinja, Homa Bay na Kisumu, ambapo taka ngumu hazizolewi kwa wakati na mvua zinaponyesha husombwa kuingia ziwani.
Pia amesema ukataji wa miti katika vyanzo vya maji umechangia mmomonyoko wa udongo na mchanga ambao husombwa na maji kuingia ziwani, hali inayoongeza kina cha maji na kusababisha baadhi ya fukwe kumezwa na maji.
Dkt. Bwire ameonya kuwa endapo hatua madhubuti hazitachukuliwa sasa, hali ya uchafuzi itaendelea kuongezeka na kuhatarisha uwepo wa ziwa hilo katika miaka ijayo.
“Kwa tafiti tunazozifanya, hali ikiendelea hivi, ndani ya miaka 50 hadi 80 ijayo tunaweza kupoteza uwezo wa kulirejesha Ziwa Victoria katika hali yake ya kawaida,” amesema Dkt. Bwire.

