Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso, amesema utendaji wa Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za Maji utapimwa kwa kuzingatia uwezo wao wa kukabiliana na changamoto hiyo, akisisitiza kuwa suala hilo ni muhimu katika kuongeza ufanisi wa huduma na mapato ya sekta.
Aweso ametoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa Taarifa ya Utendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa mwaka 2024/25, ambapo ameeleza kuwa tathmini iliyofanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) inapaswa kutumika kuleta mabadiliko ya kweli katika sekta hiyo.
Amesisitiza kuwa ni lazima mamlaka za maji zitatue changamoto ya upotevu wa maji kwa kuwa ni eneo lenye athari kubwa kiuchumi, akieleza kuwa maji yanayopotea ni sawa na fedha inayopotea.
Aidha, Waziri Aweso amehimiza matumizi ya teknolojia za kisasa katika kushughulikia changamoto mbalimbali za sekta, zikiwemo upotevu wa maji, malalamiko ya ankara, pamoja na ulinzi wa miundombinu na vyanzo vya maji.

Amesema Serikali imejidhatiti kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za majisafi na usafi wa mazingira kupitia mageuzi ya sekta na usimamizi imara wa mamlaka za maji nchini.
Pia amebainisha umuhimu wa kuwajengea uwezo watendaji wa sekta ya maji ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, pamoja na kuimarisha bodi za wakurugenzi ili kusimamia vyema taasisi hizo na kuhakikisha zinafikia malengo yaliyokusudiwa.
Kadhalika, amesisitiza haja ya kuweka mfumo rasmi wa kisheria utakaowezesha ushirikiano na uwekezaji wa sekta binafsi ili kuongeza ufanisi na rasilimali fedha katika sekta hiyo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri, amesema utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan unapaswa kuonekana kwa vitendo kupitia utendaji bora wa mamlaka za maji, akibainisha kuwa maji ni nguzo muhimu ya maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile, amesema licha ya mafanikio yaliyofikiwa, bado mamlaka za maji zina jukumu kubwa la kuboresha huduma za majisafi na usafi wa mazingira, huku akisisitiza uwajibikaji wa wakurugenzi watendaji katika usimamizi wa rasilimali watu, fedha na utekelezaji wa mipango ya taasisi kila mwaka.

Kwa ujumla, tathmini ya utendaji inaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha mamlaka zote za maji zinatoa huduma bora kwa kuzingatia ufanisi, uwajibikaji na matumizi sahihi ya rasilimali, huku mafanikio ya sekta yakipimwa kwa namna yanavyogusa maisha ya wananchi kupitia huduma bora, salama na endelevu.

