Na Lucy Lyatuu, Dodoma
WAZIRI wa Madini Anthony Mavunde ameielekeza Tume ya Madini kufuta jumla ya leseni 40 za utafiti wa madini ambao wameshindwa kuendeleza leseni hizo huku akiagiza maofisa madini kusimamia sheria ya madini ipasavyo.
AIdha amesema lipo wimbi kubwa la watu kuingia kwenye leseni za wengine hivyo ufutaji wa leseni hizo kuimarisha usimamizi wa rasilimali za madini na kuondoa wamiliki wasiotekeleza masharti ya leseni, huku akionya kuwa Serikali haitavumilia uzembe unaokwamisha maendeleo ya Sekta ya Madini pamoja na uchumi kwa ujumla.
Waziri Mavunde ameoa taarifa hiyo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari, akieleza kuwa leseni hizo zimefutwa baada ya wamiliki wake kushindwa kuziendeleza licha ya kupewa hati za makosa na muda wa kurekebisha kasoro zilizobainika na kwamba zitarudishwa Serikalini kwa ajili ya kuweka utaratibu wa kugawa kwa wachimbaji wadogo,wawekezaji walio na utayari na makundi ya Wanawake na Vijana kupitia Programu ya Mining for A Brighter Tomorrow-MBT.

Amesema kuwa, tathmini ya kina iliyofanywa na Wizara ya Madini imeonesha uwepo wa ukiukwaji mkubwa wa masharti ya leseni, ikiwemo baadhi ya wamiliki kuhodhi maeneo bila kuyaendeleza, kushindwa kulipa ada stahiki, kutotekeleza wajibu wa ushirikishwaji wa Watanzania (Local Content), pamoja na kushindwa kutekeleza miradi ya uwajibikaji kwa jamii (CSR).
Kadhalika amesema mwenye leseni ana jukumu la kulinda leseni yake na kwamba atakayeingia kwenye eneo lake aondolewe mara moja kwa mujibu wa sheria
Amesema vitendo vya kuhodhi leseni vimekuwa chanzo kikubwa cha migogoro na kuchochea uchimbaji holela, hali inayohatarisha usalama wa wananchi, mazingira na mapato ya Serikali.
Wakati huo huo serikali kupitia Tume ya Madini imetoa hati za makosa kwa leseni nyingine 43, zikiwemo leseni 40 za utafutaji na tatu za uchimbaji wa kati, huku wamiliki wake wakitakiwa kurekebisha kasoro ndani ya siku 30.
Amesisitiza kuwa endapo masharti hayo hayatatekelezwa ndani ya muda uliowekwa, leseni hizo zitafutwa na maeneo husika kutolewa kwa wawekezaji wengine wenye uwezo wa kuyaendeleza.

Mavunde amesema hatua ya kufuta leseni 40 inaashiria msimamo thabiti wa Serikali wa kuendeleza Sekta ya Madini dhidi ya uzembe na vitendo visivyo halali, huku ikifungua ukurasa mpya wa uwajibikaji na ushindani wa haki katika matumizi ya rasilimali za taifa.

