TBA Yaibuka Mshindi Bora Sekta Ya Miliki Na Majengo Na Ardhi Sabasaba

Na Lucy Lyatuu
WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) umetunukiwa tuzo ya mshindi wa nafasinya pili katika kipengele cha
banda bora upande wa Sekta ya Miliki na Majengo Na Ardhi (Real Estate) wakati wa sherehe za ufungaji wa Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Kilele cha maonesho hayo kilifikia Julai 13, 2026 katika Viwanja vya Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam zikiongozwa na Rais wa Zanzibar, na Dkt Hussein Ali Mwinyi kufunga na kutoa tuzo kwa washindi.
Aidha tuzo ya TBA imepokelewa kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa TBA, Daud Kondoro, na Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa TBA, Amina Lumuli.
Akizungumza Lumuli amesema ushindi huo unatokana na ubunifu mkubwa uliooneshwa katika maandalizi ya banda la taasisi hiyo pamoja na namna lilivyofanikiwa kuwasilisha fursa mbalimbali za uwekezaji kwa wananchi na wadau wa maendeleo.
” TBA imeweka mkazo katika kuonesha fursa za uwekezaji kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), pamoja na kuelimisha wananchi kuhusu miradi ya kimkakati inayotekelezwa na wakala huo katika maeneo mbalimbali nchini,” amesema.
Amesema miongoni mwa miradi iliyovutia wageni wengi waliotembelea banda la TBA ni pamoja na ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, miradi ya majengo ya serikali pamoja na ukarabati na uboreshaji wa miundombinu ya michezo ikiwemo Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambayo imeendelea kuonesha uwezo wa kitaalamu wa taasisi hiyo katika sekta ya ujenzi na usimamizi wa majengo.

Lumuli amesema tuzo hiyo ni ishara ya kuendelea kuaminiwa kwa TBA na wananchi pamoja na wadau mbalimbali kutokana na huduma bora, ubunifu wa kihandisi na uwezo wa taasisi hiyo wa kutekeleza miradi yenye tija kwa maendeleo ya Taifa na ustawi wa wananchi.
TBA inaendelea kutajwa kuwa miongoni mwa taasisi za serikali zinazofanya vizuri katika utoaji wa huduma, ubunifu wa kihandisi na kuvutia wawekezaji pamoja na wananchi waliotembelea maonesho hayo ya Jubilee ya Dhahabu ya Sabasaba 2026.

