Na Lucy Ngowi
DODOMA: MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeendelea kusisitiza umuhimu wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa kwa wananchi na wadau mbalimbali kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea jijini Dodoma.
Akizungumza katika banda la TMA, Ofisa Masoko wa mamlaka hiyo, Nasri Msulwa, amesema maonesho hayo yamekuwa fursa muhimu ya kutoa elimu kuhusu huduma za hali ya hewa zinazotolewa na taasisi hiyo, ikiwemo utabiri wa kila siku, utabiri wa msimu na tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa.
Amesema TMA inalenga kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati ili kuwasaidia kufanya maamuzi bora na kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na matukio mbalimbali ya hali ya hewa.

“Tunaendelea kuhamasisha matumizi ya taarifa za hali ya hewa kwa sababu zina mchango mkubwa katika kusaidia sekta mbalimbali kupanga na kutekeleza shughuli zake kwa ufanisi,” amesema Msulwa.
Amefafanua kuwa sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, usafiri wa anga na majini pamoja na usimamizi wa maafa ni miongoni mwa maeneo yanayotegemea kwa kiwango kikubwa taarifa za hali ya hewa katika kupanga shughuli na kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza.
Mbali na kutoa elimu, TMA pia imewasilisha teknolojia na mifumo mbalimbali inayotumika katika ukusanyaji, uchambuzi na utoaji wa taarifa za hali ya hewa.

Hatua hiyo imewapa wananchi nafasi ya kuelewa mchakato mzima wa utoaji wa utabiri na tahadhari za hali ya hewa.
Wananchi waliotembelea banda la mamlaka hiyo wamepongeza juhudi za TMA za kuendelea kutoa elimu kwa umma, wakieleza kuwa taarifa za hali ya hewa zimekuwa msaada mkubwa katika kupanga shughuli zao za kila siku na kujikinga dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
Ushiriki wa TMA katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ni sehemu ya jitihada za serikali za kusogeza huduma karibu na wananchi na kuongeza uelewa kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi mbalimbali za umma.








