Na Lucy Ngowi
MWALIMU wa fani ya useketaji ambayo ni utengenezaji wa vitambaa vya nguo,vikoi kutoka Mamlaka ya Mafunzo na Ufundi Stadi ( VETA), Chuo cha Tabora, Diana Mlengeki amewaasa vijana kusoma fani ambazo siyo maarufu kwa kuwa ndioi zenye fursa kubwa ya ajira.
Mlengeki amesema hayo jijiji Dodoma kwenye maonesho ya wakulima, wafugaji na Wavuvi yanayoendelea.
Amesema vijana wengi wamekuwa wakikimbilia kusoma fani ambazo ni maarufu kama vile ufundi wa magari,umeme na fani nyingine mwisho wa siku anashindwa hata kujiajiri ama kuajiriwa.
Amesema fani kama ya useketaji ambayo inafundisha kutengeneza vitambaa vya aina mbalimbali kwa kutumia nyuzi za pamba au nyuzi zozote haina umaarufu lakini ina fursa kubwa ya ajira hata za binafsi.
“Vijana wengi wanakimbilia kujifunza fani za umeme au magari ambazo ni fani maarufu kwa hiyo unakuta hata ajira ikutangazwa inahitaji watu wawili lakini waombaji wanakuwa hata zaidi ya 1,000,sasa hii ni changamoto,” amesema.
Mlengeki amesema,katika chuo hicho wana mashine ndogo na mashine kubwa ambapo unaweza kutengeneza ‘table mart’ na mitandio ambapo mashine kubwa hutumika kutengeneza vitambaa vya kushonea magauni au mashati na vikoi .
Amesema wao wamelenga kufundisha vijana wa kitanzania ili waweze kujiajiri huku akisema kama viwanda vya hapa nchini vya nguo na nyuzi vingekuwa vinafanya kazi vizuri basi wanaotoka VETA ndio wangekuwa wataalam katika viwanda hivyo.
Amesema mashine ndogo inapatikana kwa 150,000 na inaweza kutengeneza mitandio miwili kwa siku ya mita mbili mbili na mashine kubwa ambayo huuzwa kwa milioni 1.5 hutengeneza mitandio hadi saba kwa siku.