Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: SERIKALI imesema inaendelea kutumia teknolojia kama nyenzo muhimu ya kuharakisha utoaji wa huduma, kupokea maoni na kuwaunganisha vijana na fursa za kiuchumi, kijamii kwa urahisi na kwa wakati.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka amesema serikali imeanza maandalizi ya kuanzisha jukwaa la kidijitali la huduma jumuishi litakalowezesha vijana kupata taarifa za ajira, mafunzo, mikopo, masoko na huduma nyingine kwa mfumo rahisi.
Amesema pia serikali inaendelea kuimarisha majukwaa ya ushiriki wa vijana ikiwemo VIJANA Platform, linalolenga kusikiliza sauti za vijana, kujadili changamoto zao na kuwaunganisha na wadau, sambamba na kukamilisha mifumo ya kisheria ya ushiriki wa vijana ikiwemo Baraza la Vijana.
Nanauka amesema serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya ubunifu kwa vijana kupitia vituo atamizi na kulea wabunifu pamoja na kuimarisha ulinzi wa kazi za ubunifu katika sanaa, michezo, filamu na muziki ili vijana wanufaike kiuchumi.
Aidha, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana ina vituo vitatu vya maendeleo ya vijana vya Sasanda (Songwe), Ilonga (Morogoro) na Marangu (Kilimanjaro), ambavyo vimepangwa kufufuliwa na kuboreshwa ili kutoa ujuzi wa vitendo, ujasiriamali na ajira, ikiwemo kuanzisha programu ya Open Coding School kwa ujuzi wa TEHAMA.
Amesisitiza kuwa utekelezaji wa ajenda ya vijana unahitaji ushirikiano wa wadau wote wakiwemo sekta binafsi, taasisi za fedha, mashirika ya kiraia na wadau wa maendeleo.
Amewahimiza vijana kuwa wazalendo, wachapakazi na walinzi wa amani, akisisitiza kauli mbiu ya “Vijana Tuyajenge, Tanzania ni Yetu” kama wito wa vitendo katika kujenga Taifa.

