Aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu wakiwa kwenye uzinduzi wa ‘Premier Products’ uliofanyika Arusha mwaka juzi 2024
Na Lucy Ngowi
MWAKA 2015, vijana watatu wenye ndoto ya kutatua changamoto za wakulima walikuwa na wazo tu.
Hawakuwa na kiwanda, hawakuwa na mashine za kisasa wala mtaji mkubwa. Walichokuwa nacho ni ubunifu na imani kwamba teknolojia inaweza kubadilisha kilimo cha Tanzania.
Leo, miaka 11 baadaye, kampuni yao ya Imara Technology Ltd imeajiri zaidi ya watu 50, imesambaza mashine zaidi ya 2,500 ndani na nje ya Tanzania, imefikia zaidi ya wakulima 100,000 na kuuza bidhaa zake katika nchi nane za Afrika.
Nyuma ya mafanikio hayo kuna uwekezaji wa Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), taasisi inayoadhimisha miaka 40 tangu kuanzishwa kwake.

Mkurugenzi mtendaji wa Imara Tech Alfred Chengula
Mkurugenzi Mtendaji wa Imara Technology Ltd, Alfred Chengula, anasema safari yao ilianza kwa kupata ruzuku ya kwanza ya COSTECH iliyowawezesha kutengeneza mfano (prototype) wa mashine yao ya kwanza.
“Tulikuwa na wazo pekee. COSTECH ilitupa ruzuku ya kwanza iliyotuwezesha kutengeneza mashine yetu ya kwanza na kuijaribu. Baadaye tukapata ruzuku nyingine kwa ajili ya kufanya utafiti wa soko kabla ya kuingia rasmi sokoni,” anasema Chengula.
Fedha hizo hazikusaidia tu kutengeneza mashine, bali pia zilitoa ujasiri wa kuanzisha kampuni rasmi mwaka 2019.
Kutoka kwa wabunifu watatu, leo Imara Technology imekua kampuni inayotengeneza teknolojia za kilimo zinazotambulika ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Chengula anasema mashine yao maarufu ina uwezo wa kukoboa na kupura mazao tisa tofauti, yakiwemo mahindi, maharage, mtama, mbaazi, alizeti, choroko na uwele. Ubunifu huo umeondoa ulazima wa kuwa na mashine tofauti kwa kila zao, hivyo kupunguza gharama kwa na wajasiriamali.
Kampuni hiyo pia hutengeneza mashine za kutengeneza chakula cha mifugo zinazokatakata mabua, kusaga magunzi na kuandaa malighafi mbalimbali kwa ajili ya lishe ya mifugo.
Kwa mujibu wa Chengula, mafanikio hayo yasingefikiwa bila mazingira yaliyowekwa na COSTECH ya kuwalea wabunifu kutoka hatua ya wazo hadi biashara.
“Tulianza kwa ruzuku ya Sh. Milioni 20, baadaye tukapata Sh. Milioni 40 kwa ajili ya kuendeleza teknolojia yetu. Zaidi ya fedha, COSTECH ilinipa fursa ya kwenda Finland kukutana na wawekezaji. Safari hiyo ilizaa uwekezaji wa zaidi ya Sh. milioni 500 kwenye kampuni yetu,” anasema.
Kwa miaka 40, COSTECH imekuwa kiungo kati ya utafiti, ubunifu, mtaji na masoko, ikiwezesha mawazo ya Watanzania kukua na kuwa biashara zinazochangia uchumi wa taifa.
Leo, mashine za Imara Technology zimeuzwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rwanda, Uganda, Burundi, Kenya, Malawi na Zimbabwe. Zaidi ya mashine 300 zimeuzwa nje ya Tanzania, jambo linaloonyesha kuwa teknolojia ya Kitanzania inaweza kushindana katika soko la kikanda.
Chengula anasema siri ya mafanikio yao ni kubuni teknolojia zinazojibu mahitaji halisi ya wakulima. Mashine hizo ni rahisi kubebwa hata kwa pikipiki, hutumia mafuta kidogo na zina uwezo wa kukoboa gunia 25 za mahindi kwa saa kwa kutumia lita moja tu ya mafuta, huku zikimwezesha mjasiriamali kupata hadi Sh. 25,000 kwa saa.
Hata hivyo, anasema sekta ya ubunifu bado inakabiliwa na changamoto za gharama kubwa za malighafi kutokana na kodi za pembejeo na uhaba wa wataalamu wa kuendesha mashine za kisasa.
Licha ya hayo, kampuni ina mpango wa kujenga kiwanda kikubwa Dodoma kitakachoongeza uzalishaji, ajira na ushindani wa teknolojia za kilimo za Tanzania.
Lakini mafanikio ya Imara Technology hayaishii kiwandani. Yanaonekana pia mashambani, ambako teknolojia hiyo imebadili maisha ya wakulima.
Mkurugenxi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu aliwahi kunukuliwa akisema, “Teknolojia hii inawasaidia wakulima wadogo kufanya kazi kwa haraka na kuongeza kipato,”.
Pia alisifu ubunifu wa kampuni hiyo
kwa kutengeneza mashine ya kisasa ya kupuria mazao mbalimbali.

Timu ya Imara Tech ikiwa Ruvuma
Ikitoa elimu ya mashine kwa wakulima
Ikitoa elimu ya mashine kwa wakulima
Miongoni mwa wanufaika ni mkulima Raphael Mwazembe wa Wilaya ya Mbozi.
Anasema alianza kutumia mashine za Imara Technology mwaka 2018, wakati kampuni hiyo ikiwa ndiyo inaanza kujijengea jina sokoni. Tangu wakati huo, uzalishaji wake umeongezeka na biashara yake imepanuka.
“Nilipoona uwezo wake wa kufanya kazi nilikamilisha malipo na kuanza kuitumia. Baada ya muda wakulima wengine walivutiwa nayo kwa sababu wakati huo hakukuwa na mashine nyingine yenye uwezo kama huo,” anasema.
Mkulima huyo anasema, kutokana na mafanikio aliyoyapata, baadaye alinunua mashine kubwa zaidi na kuanza kutoa huduma kwa wakulima, ikiwemo nchini Kenya. Pia aliongeza mashine ya kubangua na kusaga nafaka kwa ajili ya kutengeneza chakula cha kuku na mifugo mingine.
Mwazembe, ambaye pia ni mtengenezaji wa mashine anasema mashine hizo zimemwezesha kuzalisha malisho bora na kuwavutia wakulima wengi kufuata huduma zake.
Anaongeza kuwa matoleo mapya ya mashine hizo yameboreshwa zaidi na yana uwezo mkubwa wa kuongeza uzalishaji.
Anawahimiza wakulima kutumia mashine zenye ubora uliothibitishwa, akieleza kuwa alizonunua zimeendelea kufanya kazi kwa ufanisi kwa miaka mingi.
Kwa mujibu wake, mashine hiyo ina uwezo wa kuchakata gunia moja la mahindi ndani ya takribani dakika moja, kutegemeana na kasi ya upakiaji.
Maelezo ya Mwazembe yanaonyesha kwa vitendo jinsi uwekezaji wa COSTECH ulivyosaidia kubadili wazo la wabunifu wa Kitanzania na kuwa teknolojia, inayoboresha maisha ya maelfu ya wakulima.
Kutoka kwenye ruzuku ya kutengeneza mfano wa kwanza wa mashine hadi kufikia mauzo katika nchi mbalimbali za Afrika, Imara Technology ni ushahidi kwamba uwekezaji katika sayansi, teknolojia na ubunifu unaweza kuzalisha ajira, kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi wa taifa.
Huo ndio urithi wa miaka 40 ya COSTECH kuibua vipaji, kukuza ubunifu na kugeuza mawazo ya Watanzania kuwa suluhisho zinazogusa maisha ya wananchi na kuipa Tanzania nafasi ya ushindani katika uchumi wa maarifa.
Timu ya Mafundi ya Imara Tech wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kukamilisha toleo jipya la mashine kubwa ya kuchakata chakula cha mifugo


