Na Lucy Ngowi
Sumu ya nyuki ni moja ya bidhaa adimu zenye thamani kubwa kiafya na kiuchumi duniani, lakini bado haijafahamika kwa kiwango kikubwa nchini Tanzania.
Bidhaa hiyo huvunwa kwa kutumia teknolojia maalumu bila kumuua nyuki, na hutumika katika utengenezaji wa dawa, vipodozi pamoja na tafiti mbalimbali za tiba.
Kadri dunia inavyoelekea kwenye matumizi ya teknolojia na ubunifu katika kilimo na afya, vijana wa Kitanzania wameanza kuona fursa mpya ndani ya sekta ya ufugaji nyuki kupitia uvunaji wa sumu ya nyuki.

Mkurugenzi wa kampuni ya Sensor Tanzania Ltd, Patrick Kitosi, anasema kampuni hiyo imejikita katika ubunifu wa mashine mbalimbali, ikiwemo mashine za kuvuna sumu ya nyuki kwa kutumia teknolojia ya kielektroniki.
Anasema ili kuvuna sumu hiyo, nyuki huchochewa kwa mshtuko mdogo wa umeme unaowafanya wajihami kwa kutoa sumu kwenye kifaa maalumu kilichowekwa kwenye mzinga.
Anasema sumu hiyo hukusanywa katika mfumo wa unga na kupimwa kwa gramu kabla ya kuuzwa sokoni.
“Teknolojia hii tuliianza kuifanyia utafiti tangu mwaka 2021. Tulibuni mfumo unaotumia sauti kuvuta nyuki karibu na kifaa, kisha hupata mshtuko mdogo wa umeme na kutoa sumu bila kuathiri maisha yao,” anasema Kitosi.

Kwa mujibu wake, sumu ya nyuki ina matumizi makubwa katika sekta ya afya, ikiwemo kusaidia kutengeneza dawa za magonjwa yanayohusiana na mishipa ya fahamu, misuli na baadhi ya maambukizi ya bakteria.
Anasema, nchi kama Algeria, India na China tayari zimewekeza kwa kiwango kikubwa kwenye matumizi ya bidhaa hiyo.
Kwa maelezo yake, Tanzania ina wafugaji wengi wa nyuki, lakini wengi wao wamejikita zaidi kwenye uzalishaji wa asali huku wakikosa elimu na teknolojia ya kuvuna bidhaa nyingine zenye thamani kubwa kama sumu ya nyuki, nta, gundi na chavua.
“Changamoto kubwa si ukosefu wa nyuki, bali ni ukosefu wa teknolojia na masoko. Ndiyo maana sisi tukaamua kuwekeza kwenye ubunifu wa mashine ili wafugaji waweze kunufaika zaidi,” anasema.

Mbali na kuongeza kipato, uvunaji wa sumu ya nyuki pia una mchango katika utunzaji wa mazingira.
Kitosi anaeleza kuwa baada ya nyuki kutoa sumu, hulazimika kutafuta virutubisho zaidi kutoka kwenye maua ili kurejesha nguvu zake, hali inayoongeza uchavushaji wa mimea na kusaidia uzalishaji wa mazao.
Ubunifu huo unaonekana kwenda sambamba na dira ya maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2050 inayolenga kujenga uchumi wa kisasa unaotegemea maarifa, teknolojia na ubunifu.
Kupitia teknolojia hiyo, vijana wanapata ajira katika utengenezaji wa vifaa, huku wafugaji wakiongeza thamani ya shughuli zao.
Mwaka 2022, wabunifu hao walipata *mwega* wa Sh. Milioni 28 kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa ajili ya kuendeleza utafiti na utengenezaji wa vifaa hivyo.
Kitosi anasema soko la sumu ya nyuki lipo zaidi nje ya nchi kutokana na matumizi makubwa ya bidhaa hiyo katika viwanda vya dawa.

Hata hivyo, anabainisha kuwa wafugaji wengi bado wanahitaji kusaidiwa kupata masoko na elimu ya namna ya kuhifadhi bidhaa hiyo, kwani huhitaji mazingira yenye ubaridi ili isiharibike.
Anasema mzinga mmoja unaweza kutoa hadi gramu 1.5 za sumu kwa uvunaji mmoja, na mfugaji anaweza kuvuna mara kadhaa kwa mwezi endapo atatumia teknolojia sahihi.
Kwa sasa, kampuni hiyo inaendelea kuunganisha wafugaji na masoko huku ikihamasisha Watanzania kuona ufugaji nyuki kama biashara ya kisasa yenye bidhaa nyingi zaidi ya asali pekee.
Kadri dunia inavyohitaji bidhaa za asili kwa matumizi ya afya na tiba, ubunifu wa kuvuna sumu ya nyuki unaweza kuwa moja ya fursa mpya zitakazoibadilisha sekta ya ufugaji nyuki nchini na kuongeza mchango wake katika uchumi wa Taifa.

