
Kutoka Wazo Hadi Mafanikio
Kisasa Design ni kampuni ya Kitanzania inayojishughulisha na huduma za interior design, utengenezaji wa samani za kisasa, pamoja na kazi mbalimbali za chuma. Kampuni hii ilianzishwa kwa maono ya kuziba pengo lililokuwepo katika sekta ya usanifu wa ndani na samani nchini Tanzania.
Akizungumza kuhusu safari ya kampuni hiyo, Mkurugenzi wa Kisasa Design alisema kuwa waliona fursa kubwa katika soko ambapo wateja wengi, hasa wa sekta ya hoteli, walilazimika kutafuta huduma za wabunifu kutoka nje ya nchi, hususan Afrika Kusini.
“Tuliona kuna nafasi kubwa sana kwenye hii industry. Watu wengi walikuwa wanaagiza interior designers kutoka nje ya nchi. Sisi tukaja na suluhisho la ndani ambalo linaweza kufanya kila kitu kuanzia design mpaka furniture production,” alisema.
Suluhisho la Ndani kwa Mahitaji ya Ndani
Kupitia uwekezaji katika ubunifu na teknolojia, Kisasa Design imeweza kuondoa utegemezi wa wataalamu wa nje kwa kutoa huduma kamili zinazojumuisha usanifu wa ndani, utengenezaji wa samani na kazi za chuma kwa viwango vya kimataifa.
Kampuni hiyo imekuwa ikihudumia wateja wa aina mbalimbali huku ikihakikisha kila mradi unapata muonekano wa kipekee unaoakisi mahitaji na hadithi ya mteja husika.

Ajira kwa Watanzania
Mbali na kutoa huduma bora, Kisasa Design imechangia kwa kiasi kikubwa katika kuunda ajira kwa Watanzania.
Kwa sasa kampuni ina timu ya wabunifu wa ndani zaidi ya kumi ambao wote ni Watanzania. Aidha, zaidi ya wafanyakazi mia moja wanashiriki katika shughuli za utengenezaji wa samani, huku wengine wakifanya kazi katika idara za ofisi, mauzo na masoko.
Hatua hii imechangia kukuza ujuzi wa wataalamu wa ndani na kuimarisha sekta ya ubunifu nchini.
Ubunifu Unaotokana na Hadithi ya Mteja
Kisasa Design inaamini kuwa kila mradi una hadithi yake ya kipekee. Kwa msingi huo, kampuni hutengeneza michoro na miundo inayochochewa na mahitaji, maono na hadithi ya kila mteja.
“Tunaamini kwamba kila project ina story yake, hivyo design tunayotoa inatokana na kile kinachomhamasisha mteja wetu,” alisema mkurugenzi huyo.
Mustakabali wa Sekta
Ukuaji wa Kisasa Design unaonesha jinsi kampuni za Kitanzania zinavyoweza kushindana na kutoa huduma za kiwango cha kimataifa. Kupitia ubunifu, uwekezaji katika rasilimali watu na kuamini vipaji vya ndani, kampuni hiyo imeendelea kuwa mfano wa mafanikio katika sekta ya interior design na furniture production nchini Tanzania.

