Na Lucy Ngowi
Dodoma:WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umewataka wafanyabiashara nchini kuhakikisha wanarasimisha biashara zao kwa kuzisajili rasmi ili kuongeza fursa za ukuaji, kupata masoko mapya na kuimarisha ushindani wa biashara zao.
Wito huo umetolewa na Ofisa Usajili wa BRELA, Yusuph Mwasakafyuka, wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Amesema usajili wa biashara una manufaa makubwa kwa wafanyabiashara kwani huwapa utambulisho rasmi, hulinda chapa zao za biashara na kuwajengea uaminifu kwa wateja pamoja na wadau wengine wa maendeleo.
Mwasakafyuka amesema BRELA inatumia maonesho hayo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo, sambamba na kusajili biashara na kutoa vyeti papo kwa papo kwa waombaji wanaokidhi vigezo.
Ameeleza kuwa taasisi hiyo inasimamia sheria zinazohusu usajili wa makampuni, majina ya biashara, alama za biashara, leseni za viwanda, leseni za biashara za Kundi A na usajili wa hataza.
Kwa mujibu wake, mwitikio wa wananchi umeendelea kuongezeka tangu kuanza kwa maonesho hayo, ambapo mamia ya watu wamejitokeza kupata huduma na ushauri kuhusu usajili wa biashara na masuala mengine yanayohusiana na urasimishaji wa shughuli za kiuchumi.
Aidha, amesema wataalamu wa BRELA wamekuwa wakitoa msaada kwa wateja wanaokabiliwa na changamoto katika matumizi ya mfumo mpya wa usajili, hususan wale waliowasilisha taarifa zisizo sahihi wakati wa kujisajili.
Amesisitiza kuwa biashara zilizosajiliwa huwa na nafasi kubwa ya kupata huduma za kifedha kutoka benki na taasisi nyingine za mikopo, jambo linalosaidia kuongeza mtaji na kupanua shughuli za uzalishaji.
“Urasimishaji wa biashara ni hatua muhimu katika kujenga biashara imara na yenye uwezo wa kushindana katika soko la ndani na nje ya nchi,” amesema.

