Na Lucy Lyatuu, Dodoma
WIZARA ya Nishati imewasilisha mpango na bajeti ya kwa mwaka wa fedha 2026/27 na kuhakikisha nchi ina uhakika wa upatikanaji wa nishati ya kutosha, ya uhakika na nafuu kwa matumizi ya ndani na ziada ya kuuza nje.
Aidha Wizara hiyo imeomba kuidhinishiwa zaidi ya Sh trilioni 2.5, huku ikiweka wazi vipaumbele 10 vitakavyoongoza sekta hiyo kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi, kuimarisha upatikanaji wa nishati na kuboresha maisha ya wananchi.
Aidha, Serikali imepanga kuanzisha hifadhi ya kimkakati ya mafuta ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya bei na upatikanaji wa mafuta duniani.
Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi amesema hayo wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Nishati Kwa mwaka 2026/27 katika Bunge na kuongeza kuwa maandalizi ya bajeti hiyo yamezingatia nyaraka muhimu za kitaifa ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na Mpango wa Nne wa Maendeleo ya Taifa (FYDP IV).
Amesema Bajeti Ina lengo kuu la kuhakikisha nchi ina uhakika wa upatikanaji wa nishati ya kutosha, ya uhakika na nafuu kwa matumizi ya ndani na ziada ya kuuza nje,” alisema.
Amesema kati ya fedha hizo, asilimia 97.5 sawa na zaidi ya Sh trilioni 2.46 zitaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo, huku asilimia 2.5 sawa na zaidi ya Sh bilioni 63 zikitumika kwa matumizi ya kawaida.
Kuhusu mafuta amesema hatua hiyo imechochewa na changamoto za kimataifa zikiwemo migogoro ya kisiasa na vita katika nchi zinazozalisha mafuta, hali inayosababisha kuyumba kwa bei na upatikanaji wa bidhaa hizo.
“Serikali inakusudia kujenga kituo kikubwa cha kuhifadhi mafuta Dar es Salaam ili kuhakikisha usalama na uhakika wa upatikanaji wa mafuta nchini na nchi jirani,” amesema.
Amevitaja vipaumbele Kwa Wizara hiyo kuwa ni kuimarisha uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme; kuongeza kasi ya kuunganisha umeme kwa wananchi; kuimarisha Gridi ya Taifa; kufanya matengenezo ya miundombinu ya umeme; na kusambaza umeme vijijini na vitongojini.
“Vipaumbele vingine ni kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia; kuimarisha uzalishaji wa gesi asilia; kuhakikisha upatikanaji wa mafuta; kuboresha miundombinu ya uhifadhi na usafirishaji wa nishati; pamoja na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika uwekezaji wa nishati,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Ndejembi ametangaza utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati itakayoongeza uzalishaji wa umeme na kuimarisha miundombinu ya nishati nchini.
Ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni Mradi wa Umeme wa Maji wa Julius Nyerere wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115, mradi wa Kinyerezi III (MW 1,000), mradi wa umeme jua Shinyanga (MW 150) pamoja na miradi ya Malagarasi, Kakono, Ruhudji, Rumakali na Kikonge.
Amesema miradi hiyo inalenga kuongeza uzalishaji wa umeme ili kukidhi mahitaji ya ndani na kuwezesha kuuza umeme nje ya nchi, hatua itakayosaidia kuingiza fedha za kigeni.
Kuhusu Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Serikali itaendelea kusambaza umeme vijijini na vitongojini kupitia miradi ya Last Mile Connectivity pamoja na awamu mbalimbali za miradi ya HEP, ambapo kaya zaidi ya 200,000 zinatarajiwa kunufaika na nishati safi ya kupikia.
Waziri Ndejembi amesema Serikali pia inaendelea kupanua matumizi ya gesi asilia nchini kwa kujenga miundombinu ya usambazaji katika maeneo mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Mtwara, Lindi pamoja na mikoa mingine.
Amesema katika Jiji la Dar es Salaam, mradi wa usambazaji wa gesi utahusisha maeneo ya Ubungo, Sinza, Mikocheni na Lugalo pamoja na kuunganisha wateja wapya 1,000.
Kuhusu mafanikio yaliyopatikana yanaonesha kuwa kiwango cha upatikanaji wa umeme nchini kimeongezeka kutoka asilimia 78.4 mwaka 2020 hadi asilimia 85.5, huku kiwango cha wananchi waliounganishiwa umeme kikiongezeka kutoka asilimia 37.7 hadi asilimia 52.1.
Amesema Serikali inalenga kuunganisha wateja wapya milioni 8.3 ili kufikia asilimia 75 ya wananchi waliounganishiwa umeme ifikapo mwaka 2030.
“Maendeleo ya taifa lolote yanategemea upatikanaji wa nishati ya uhakika na nafuu. Ndiyo maana Serikali inaendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta hii,” amesisitiza.

