Na Mwandishi Wetu
WATENDAJI Wakuu wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali wameagizwa kuhakikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inakuwa msingi wa maamuzi, mipango na bajeti za taasisi wanazoziongoza ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Agizo hilo limetolewa Julai 24, 2026 mjini Kibaha, mkoani Pwani, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, wakati akifunga mafunzo ya siku tatu kwa Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma yaliyolenga kuimarisha uongozi na utendaji.
Ridhiwani amesema kuwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ulianza rasmi Julai Mosi mwaka huu 2026, hivyo kila taasisi inapaswa kuoanisha mipango yake ya kimkakati, bajeti na vipaumbele na malengo ya dira hiyo.

Amesisitiza kuwa mafanikio ya Dira 2050 hayatapatikana kwa matamko pekee, bali kupitia maamuzi ya kila siku ya viongozi wa taasisi za umma.
Amesema kila bajeti, mradi, uwekezaji na huduma inayotolewa inapaswa kuonyesha mchango wake katika kufanikisha malengo ya dira hiyo.
Pia amewataka Watendaji Wakuu kuhakikisha viashiria vya utendaji vya taasisi zao vinaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili kurahisisha upimaji wa mchango wa kila taasisi katika utekelezaji wake na kuimarisha uwajibikaji.

“Nina imani kuwa maarifa na uzoefu mlioupata utatafsiriwa katika utendaji wenye matokeo chanya, hivyo kuimarisha utawala bora, kuongeza ufanisi wa Taasisi za Umma na kuharakisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa manufaa ya maendeleo endelevu ya Taifa,” amesema Ridhiwani.
Ridhiwani aliipongeza Ofisi ya Msajili wa Hazina, Taasisi ya Uongozi na wadau mbalimbali kwa maandalizi na uratibu wa mafunzo hayo, akisema yamewajengea uwezo Watendaji Wakuu kuongoza taasisi kwa ufanisi, kuongeza tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi na kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Serikali.

