WIZARA Ya Ardhi, Nyumba Na Maendeleo Ya Makazi imesema kutokulipa kodi ya pango la ardhi ni kosa ambalo linaweza kusababisha kukosa sifa ya kukopesheka katika taasisi za fedha, na vile vile kukosa sifa za kugombea nafasi za Uongozi ikiwemo Udiwani na Ubunge.
Aidha katika mwaka 2026/27, Wizara imepanga kukusanya sh bilioni 300 kutokana na kodi ya pango la ardhi, ada na tozo mbalimbali zinazohusiana na sekta ya ardhi.
Waziri wa wizara hiyo, Dkt leonard Akwilapo amesema hayo wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara hiyo Bungeni na kuiomba kuidhinishiwa sh bilioni 210.2 kwa mwaka 2026/27 kwa ajili ya utekelezaji vipaumbele vya Wizara.
Ametoa rai kwa wamiliki wote wa ardhi kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao wa msingi wa kulipa kodi ya pango la ardhi, kwa wakati, ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kufutiwa umiliki.
Kuhusu kukusanya kodi lengo hilo litafikiwa kwa kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo kuendelea kusambaza miundombinu na mifumo ya TEHAMA katika Ofisi za Ardhi za Mikoa na Halmashauri ili kurahisisha utoaji wa huduma za ardhi.
Amesema pia kuendelea kushirikiana na TAMISEMI kufuatilia halmashauri ambazo hazijakamilisha utekelezaji wa miradi ya KKK; na kuchukua hatua za kisheria kwa wadaiwa sugu ikiwemo kuwafikisha mahakamani.
Aidha, amesema Wizara kwa kushirikiana na mamlaka nyingine inaendelea kutafuta njia bora ya ukusanyaji wa kodi ya pango la ardhi kupitia huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi hizo.
Kuhusu hati na nyaraka za Kisheria amesema , katika mwaka 2025/26, Wizara ilipanga kuandaa na kusajili Hatimiliki 500,000, Hati za Hakimiliki ya Kimila 520,000, Hati za Sehemu ya Jengo 1,000, Vyeti vya Ardhi ya Kijiji 100 na Miamala ya Hatimiliki na Nyaraka za Kisheria 100,000.
Amesema hadi Mei 15, 2026 Wizara imeandaa na kusajili Hatimiliki 107,683 sawa na asilimia 21.54 ya lengo; Hati za Hakimiliki ya Kimila 99,762 sawa na asilimia 19.19 ya lengo; Vyeti vya Ardhi ya Kijiji 148 sawa na asilimia 148 ya lengo; na Hati za Sehemu ya Jengo 914 sawa na asilimia 91.4 ya lengo.
Aidha,amesema jumla ya Miamala ya Hatimiliki na Nyaraka za Kisheria 137,681 zimesajiliwa sawa na asilimia 137.68 ya lengo.
Katika mwaka 2026/27, Wizara imepanga kuandaa na kusajili Hatimiliki 200,000, Hati za Hakimiliki ya Kimila 300,000, Vyeti vya Ardhi ya Kijiji 60, Hati za Sehemu ya Jengo 1,000 na Miamala ya Hatimiliki na Nyaraka za Kisheria 100,000.
Ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanamiliki ardhi zao kisheria ili kuepuka migogoro na kuwawezesha kutumia ardhi kwa ajili ya kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Amesema katika mwaka 2025/26, Wizara ilipanga kutatua migogoro ya ardhi 3,000. Ambapo hadi Mei 15,2026 jumla ya migogoro ya ardhi 5,573 imetatuliwa ambapo kati ya hiyo, migogoro 3,183 imetatuliwa kupitia kliniki za ardhi na migogoro 2,390 imetatuliwa kupitia utaratibu wa kawaida wa kiutawala.
Amesema katika mwaka 2026/27, Wizara imepanga kushughulikia migogoro 4,000 kiutawala na kutoa rai kwa viongozi, watumishi na wananchi kwa ujumla kuzingatia sheria za ardhi, kanuni na miongozo ili kuepuka kuanzisha migogoro mipya.