Na Lucy Ngowi
MBUNGE wa Jimbo la Ngorongoro, Yanick Ndoinyo, amesema ipo haja kwa Serikali kuweka mikakati ya kuhakikisha wananchi wa kawaida wananufaika moja kwa moja na shughuli za utalii kupitia huduma zinazotolewa vijijini.
Ndoinyo amesema kwa sasa sekta ya utalii imeendelea kuwa na manufaa makubwa ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa, huku hoteli nyingi za kitalii zenye hadhi ya nyota tatu hadi tano zikijengwa ndani ya maeneo hayo, jambo linalowafanya wananchi wengi kushindwa kupata faida ya moja kwa moja kutokana na uwepo wa watalii.
Ametoa kauli hiyo alipokuwa akichangia hotuba ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuhusu sekta ya uhifadhi, utalii na ufugaji bungeni.
Amesema ni muhimu kwa wizara hiyo kuanza kuandaa sera na mikakati itakayosaidia kurudisha miundombinu ya utalii katika maeneo ya wananchi ili kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi zinazotokana na utalii.
“Watalii walale katika gesti zetu, wanywe chai zetu na wale maandazi yetu. Hapo ndipo mwananchi wa kawaida ataona manufaa ya moja kwa moja ya utalii na fedha zitaingia katika uchumi wa wananchi,” amesema.
Aidha, Ndoinyo amesema Tanzania ina uwezo mkubwa wa kuongeza idadi ya watalii kuliko ilivyo sasa kutokana na rasilimali zilizopo pamoja na dhamira ya Serikali kuimarisha sekta hiyo.
Amesema lengo la kufikia watalii milioni nane si kubwa kwa Tanzania na linaweza kufikiwa kwa haraka ikiwa juhudi za pamoja zitaendelea kuimarishwa.

