Lucy Ngowi, Mwanza
MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amesema zaidi ya watu milioni 45 wanaoishi katika ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wananufaika na uwepo wa Ziwa Victoria, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha rasilimali hiyo muhimu inalindwa na kutunzwa kwa mipango endelevu.
Mtanda amesema hayo wakati wa uzinduzi wa maonesho yanayoambatana na maadhimisho ya Siku ya Ziwa Victoria, ambayo kilele chake kitafanyika Alhamisi, Mei 21, 2026 jijini Mwanza.
Amesema Siku ya Ziwa Victoria ilianzishwa baada ya mawaziri wa sekta za Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na wakuu wa nchi wanachama kukubaliana kuwa na maadhimisho hayo kila mwaka ifikapo Mei 21 kwa lengo la kuhamasisha uhifadhi na matumizi endelevu ya ziwa hilo.
Amesema, kwa mara ya kwanza maadhimisho hayo yanafanyika Mwanza, nchini Tanzania, jambo ambalo amesema ni heshima kubwa kwa nchi.
Ameshukuru Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa kwanza wa maadhimisho hayo muhimu.
Mtanda amesema Ziwa Victoria ni rasilimali kubwa ambayo Mungu ameijalia Afrika Mashariki, huku Tanzania ikimiliki asilimia 51 ya eneo lote la ziwa hilo, Uganda asilimia 43 na Kenya asilimia sita.
Ameongeza kuwa Bonde la Ziwa Victoria linaenea hadi Burundi na Rwanda, likiwezesha shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Ametaja shughuli zinazonufaika na ziwa hilo kuwa ni pamoja na kilimo, ufugaji, uvuvi, utalii, uhifadhi wa wanyamapori pamoja na usafirishaji.
Aidha, amesema Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki imeleta mradi mkubwa wa uokozi wenye thamani ya zaidi ya Sh Bilioni tano, ukiwa na boti na vifaa vya kisasa vya uokoaji ili kuongeza usalama ndani ya ziwa.
Akizungumzia kauli mbiu ya mwaka huu ya “Maji Yetu, Mustakabali Wetu tuungane kwa usimamizi endelevu wa Bonde la Ziwa Victoria,” Mtanda amesema mustakabali wa maisha ya binadamu na maendeleo ya kiuchumi na kijamii unategemea upatikanaji wa maji, hivyo kuna umuhimu wa kuunganisha nguvu katika kulinda na kuhifadhi Ziwa Victoria.
Amesema wananchi wa Mwanza wameanza kuchukua hatua za kuhifadhi vyanzo vya maji ikiwemo eneo la Butimba, huku serikali ikiendelea kudhibiti changamoto ya gugu maji ambayo iliwahi kuathiri shughuli za kiuchumi ndani ya ziwa hilo.
Mtanda ameongeza kuwa uchumi wa vizimba vya samaki unaendelea kukua mkoani Mwanza, lakini akasisitiza kuwa uchafuzi wa ziwa unaweza kuathiri uzalishaji huo pamoja na upatikanaji wa maji ya kutosha kwa wananchi.
Katika kilele cha maadhimisho hayo, wageni mbalimbali kutoka mikoa ya ukanda wa Ziwa Victoria wanatarajiwa kushiriki katika shughuli hiyo muhimu.

