Na Lucy Lyatuu, Dodoma
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeipokea kwa uzito mkubwa ripoti ya Tume ya Uchunguzi iliyoundwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku kikieleza kuwa mapendekezo yaliyotolewa ni msingi wa kuliponya taifa na kuimarisha umoja wa Watanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari Dodoma Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi amesema CCM inatambua umuhimu wa ripoti hiyo katika kutathmini matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea Oktoba 29, 2025.
Amesema Chama kimechukua fursa hiyo kumpongeza kwa dhati Mwenyekiti wa CCM na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uamuzi wake wa kishujaa wa kuunda tume hiyo kwa mujibu wa Sheria ya Tume za Uchunguzi (Sura ya 32).
“Tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa maono yake. Tume hii imefanya kazi kwa uhuru, weledi, na uzalendo wa hali ya juu, jambo ambalo linaonyesha ukomavu wa demokrasia yetu,” amesema Katibu huyo.
Aidha, CCM imemwagia sifa Tume hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Mkuu Mstaafu Mohammed Othman Chande, kwa namna walivyotekeleza majukumu yao kwa weledi mkubwa na kuzingatia maslahi mapana ya nchi.
Ameongeza kuwa Tume hiyo ilifanya kazi kwa weledi wa hali ya juu na kwamba CCM inaunga mkono mapendekezo yaliyotolewa na Tume hiyo na itaendelea kutoa ushirikiano wa ,ila hali pindi itakapohitajika.
Kuhusu maridhiano Chama kinatoa wito kwa makundi yote kutoa ushirikiano katika mazungumzo na maridhiano na kukubaliana kama nchi ili kuondoa mpasuko ndani ya nchi.

