Na Mwandishi Wetu
VIONGOZI wa Serikali za Mitaa nchini wametakiwa kuimarisha ushirikiano na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) katika kuanzisha na kuendesha Mifuko ya Elimu ya Halmashauri ili kuongeza kasi ya maendeleo ya sekta ya elimu.
Wito huo umetolewa wakati wa Mkutano Mkuu Maalum wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT) uliofanyika Aprili 22, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), ambapo TEA iliwasilisha mada kuhusu nafasi yake katika kukuza elimu kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa.
Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Dkt. George Mofulu, Meneja wa Utafutaji Rasilimali na Hamasa aliwasilisha mada hiyo, akieleza mafanikio yaliyopatikana.
Alibainisha kuwa katika kipindi cha 10 (2014/15–2024/25), jumla ya miradi 1,711 yenye thamani ya Sh. Bilioni 128.5 imetekelezwa kupitia mfuko huo.
Aidha, TEA ilikumbusha utekelezaji wa Waraka wa Serikali Na. 1046 na 1047 wa mwaka 2020 unaozitaka Halmashauri kuanzisha na kusimamia Mifuko ya Elimu.
Hata hivyo, tathmini ya mwaka 2025 imeonesha kuwa zaidi ya asilimia 76 ya Halmashauri bado hazijatekeleza kikamilifu agizo hilo.
Kutokana na hali hiyo, mamlaka hiyo imesisitiza umuhimu wa Halmashauri kuchukua hatua za haraka kuanzisha mifuko hiyo ili kuongeza vyanzo vya ndani vya rasilimali na kuimarisha maendeleo ya elimu kupitia ushirikiano na wadau wa ndani.
Akihitimisha, Dkt. Mofulu alisema TEA ipo tayari kushirikiana na Halmashauri zote nchini kuhakikisha mifuko hiyo inaanzishwa na kuendeshwa kwa ufanisi.

