Na Lucy Lyatuu,Dodoma
SERIKALI imesema bado kuna changamoto ya ufaulu kwa baadhi ya masomo nchini hususani somo la hisabati na kuwataka wadau wote wanaohusika kuongeza jitihada.
Imesema somo la Hisabati limekuwa shida ya Taifa na kuomba Baraza La Mtihani La Tanzania (NECTA) Kwa pamoja na wadau wote wa elimu nchini kuongeza juhudi ili kuondoa kadhia hiyo.
Naibu Waziri wa Elimu ,Sayansi Na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir amesema hayo Leo jijini Dodoma katika hafla ya uwasilishaji wa taarifa ya tathmini ya ufundishaji na ujifunzaji ngazi ya elimu msingi .

Taarifa hiyo imewasilishwa na NECTA, na kuwahusisha wadau mbalimbali wa elimu wakiwemo wadhibiti ubora wa elimu,, maofisa elimu mkoa, Wilaya,kata, walimu Wakuu, walimu pamoja na wadau mbalimbali.
Akizungumza Wanu amesema kutokana na tafiti hizo kila baada ya muda Taifa linahitaji kuimarika kwenye ufaulu wa masomo mbalimbali na kwamba ipo haja ya wadau kuongeza ushirikiano katika hatua hiyo.

“Somo la hesabu ni shida ya Taifa,kuna haja ya kuwepo Kwa hatua ambazo zitafanyika Ili kuondoa kadhia hiyo,” amesema Wanu na kuongeza kuwa hata yeye binafsi somo hilo lilimpa shida sana lakini familia iligundua anaweza kusoma taaluma nyingine ya sheria.
Amesema pamoja na tafiti kuonesha kuimarika Kwa ufaulu Kwa baadhi ya masomo lakini pia walimu Wakuu wazingatie ufundishaji wa umahiri na matumizi ya lugha yazingatiwe huku wazazi pia wakishiriki katika kuongeza ufaulu.
Wanu ameipongeza NECTA Kwa kufanya tathmini hiyo na kwamba kazi ni nzuri inayohitaji majibu ya tafiti hiyo Kufanyiwa kazi ili kuimarisha ufaulu nchini.
Amesema mapendekezo yaliyotolewa yamechukuliwa na Wizara ya Elimu,Sayansi Na Teknolojia na kwamba yatafanyiwa kazi ili Kwa tathmini hiyo matokeo yawe yamepuga hatua.
Akiwasilisha tathmini hiyo,Katibu Mtendaji wa NECTA,Profesa Said Ally Mohamed amesema tafiti ni jambo muhimu inayolifanya Taifa kujitambua liko katika hali gani kwenye ufaulu wa Wanafunzi nchini.
Amesema hali ya ufaulu haijabadilika na kwamba Kwa mwaka jana Baraza limepima kupitia mtaala mpya ambapo kwa sasa wanafunzi wote wa darasa la tatu wasiojua kusoma na kuandika wametambuliwa na kwamba haitarajiwi kufika darasa la nne wakiwa bado na hali hiyo.
Amesema wanafunzi hao wanajulikana kuanzia shuleni,kata husika,Wilaya ,mkoa na Taifa hivyo asilimia hiyo 10 ya wasiojua kusoma na kuandika wapewe masomo ya ziada wakiwa darasa la tatu na sio kusubiria kufika darasa la nne.

” Kwa mantiki hiyo itakuwa ni aibu endapo watakuwepo wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika watakaofika darasa la Saba Kwa kuwa wametambuliwa mapema,” amesema Profesa Said na kuongeza kuwa Kwa kidato cha sita hali imeendelea kuwa bora na kwamba wanafaulu Kwa kiwango cha juu huku somo la Kiwashili likifanya vizuri Kwa kidato cha pili na nne.
Profesa Said ameongeza kuwa somo la Kiingereza Kwa kidato cha pili limeendelea kuimarika mwaka hadi mwaka huku masomo ya sanaa ufaulu ukianzia chini lakini kufikia kidato cha nne ukiimarika.
“Kwa mantiki hiyo mtihani ya upimaji inayofanywa kimkoa na kitaifa unasaidia lakini Kwa somo la Hisabati hakuna mkoa ambao ufaulu wake umeweza kufikia asilimia 40,” amesema.

