Na Lucy Ngowi
DODOMA: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amewasilisha rasmi hotuba ya mapendekezo ya bajeti ya ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27, akieleza mwelekeo wa mapato, matumizi na vipaumbele vya maendeleo.
Akiwasilisha bungeni, Profesa Mkumbo amesema kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina (Fungu 007), Serikali imepanga kukusanya na kuchangia Sh. Trilioni 1.79 katika Mfuko Mkuu wa Serikali kutoka vyanzo visivyo vya kodi.
Vyanzo hivyo ni pamoja na gawio, michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi ya taasisi za umma, mapato ya Mfumo wa Usimamizi wa Mawasiliano ya Simu (TTMS), riba za mikopo, pamoja na mapato mengineyo.
Kwa upande wa matumizi, amesema Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji pamoja na taasisi zake zinaomba kuidhinishiwa jumla ya Sh. Bilioni 144.85, ambapo kati ya hizo Sh. Bilioni 126.01 ni kwa matumizi ya kawaida na Sh. Bilioni 18.83 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Katika mwaka huo wa fedha, ofisi imeweka mkazo katika kuimarisha sekta binafsi kama injini ya ukuaji wa uchumi.
Profesa Mkumbo amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, akibainisha kuwa mafanikio ya mageuzi ya uchumi yatategemea uimara, ushindani na ushiriki mpana wa wadau wote.
Amesema juhudi zitaelekezwa katika kuwawezesha wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa (MSMEs), pamoja na vijana, wanawake na makundi maalum ili kushiriki kikamilifu katika uchumi.
Aidha, ofisi itaandaa Taarifa ya Hali ya Sekta Binafsi ili kusaidia maamuzi ya sera na mipango kwa kuzingatia takwimu sahihi.
Sambamba na hilo, amesema Serikali itaboresha mfumo wa majadiliano kati yake na sekta binafsi ili kuhakikisha uwakilishi jumuishi na wenye matokeo chanya kwa maendeleo ya taifa.
Katika juhudi za kupunguza umasikini, ofisi imepanga kuratibu na kufanya tathmini ya programu zote za kupunguza umasikini nchini.
Pia itaandaa Mfumo wa Kitaifa wa Ufuatiliaji wa Umaskini utakaoweka viashiria, ukusanyaji wa takwimu na matumizi yake katika kupanga sera na bajeti.
Amesisitiza kuwa hatua hizo zinalenga kuhakikisha ukuaji wa uchumi unaenda sambamba na ustawi wa wananchi wote.

