Na Mwandishi Wetu
WIZARA ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeanza kuweka utaratibu wa kuvuna maarifa na uzoefu wa Mabalozi Wastaafu ili kuimarisha diplomasia na maendeleo ya taifa katika sekta mbalimbali.
Hatua hiyo imeelezwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, wakati akifungua kikao cha mashauriano kati ya uongozi wa wizara na Mabalozi Wastaafu kilichofanyika jijini Dar es Salaam Aprili 15, 2026.

Amesema wizara imeanzisha vikao vya mara kwa mara na Mabalozi hao kwa lengo la kutumia uzoefu wao katika kukuza uhusiano wa kimataifa utakaonufaisha nchi kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Balozi Kombo ametaja baadhi ya maeneo yanayohitaji mchango wao kuwa ni pamoja na kuimarisha biashara kati ya Tanzania na nchi nyingine, hususan barani Afrika, pamoja na kusaidia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kukuza uchumi kwa kasi na ufanisi.

Ameongeza kuwa mabadiliko ya dunia, hasa katika teknolojia ya kidigitali, yanahitaji mikakati madhubuti ili taifa linufaike na kukabiliana na changamoto zake.
Pia amesisitiza umuhimu wa uzoefu wao katika kuchambua siasa za kimataifa ambazo zimekuwa na mwelekeo usiotabirika, hali inayoweza kuathiri nchi zinazoendelea.
Aidha, amesema maarifa ya Mabalozi Wastaafu ni muhimu katika kuendeleza taswira chanya ya Tanzania kimataifa, hususan wakati nchi inapopewa majukumu ya uongozi wa kikanda na kimataifa.

Amebainisha kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika mwaka 2028, hivyo maandalizi bora yanahitajika.
Awali, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, amesema serikali inaangalia uwezekano wa kuweka mfumo rasmi wa ushirikishwaji wa Mabalozi Wastaafu kupitia Ofisi ya Rais – UTUMISHI ili mchango wao utambulike kisheria.

