Na Mwandishi wetu
DODOMA: CHAMA cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) kimewapongeza Makatibu wa Mikoa na Mawakili wa Kanda kwa utendaji wao katika kutoa huduma kwa Wanachama, huku kikitaja mchango wao kuwa ni sehemu kuu ya utekelezaji wa majukumu ya Chama nchini.
Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti TALGWU Taifa na Rais wa TUCTA, Cde. Tumaini Nyamhokya wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kupanga malengo ya utendaji kwa mwaka 2026 yaliyofanyika jijini Dodoma.

Mafunzo hayo ya siku tatu, yalianza Februari 05, 2026 na kufungwa jana Februari 07, 2026, yalilenga kuongeza ufanisi wa watendaji katika utekelezaji wa majukumu yao na kuhakikisha Watendaji hao wanaendelea kutoa huduma bora kwa Wanachama.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Cde. Nyamhokya amesema TALGWU inajivunia kuwa na watendaji wenye weledi na wanaotekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Ameongeza kuwa mchango wa watendaji hao umeimarisha imani ya Wanachama, kuongeza mshikamano katika Chama na kuweka misingi thabiti ya utekelezaji wa malengo ya mwaka 2026.




