Na Danson Kaijage, Dodoma
RAIS Samia Suluhu Hassan, amewataka majaji na mahakimu nchini kulinda haki, amani na utulivu kwa mustakabali wa Taifa.
Rais Samia alitoa agizo hilo wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (TMJA) uliofanyika jijini Dodoma.
Alisisitiza umuhimu wa watoa haki kusimamia misingi ya haki kwa kuzingatia sheria, maadili na viapo vyao bila hofu wala upendeleo.

Alisema Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025/2050 imejengwa juu ya misingi ya utawala bora, amani, usalama na utulivu, na kwamba mhimili wa Mahakama una nafasi muhimu katika kulinda misingi hiyo.
Aliongeza kuwa Serikali imeanza kuchukua hatua za kuijenga Mahakama imara, inayoaminika na kuheshimika ndani na nje ya nchi.
Akizungumzia changamoto za watumishi wa Mahakama, Rais Samia aliwataka kuwa wavumilivu, akibainisha kuwa Serikali inaendelea kushughulikia maslahi yao hatua kwa hatua.
Aidha, alisema Watanzania wana matumaini makubwa kwa majaji na mahakimu kuona haki, uwazi na utu vikitendeka kwa vitendo.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, George Masaju, aliwasilisha mapendekezo ya TMJA ikiwemo kuboreshwa kwa maslahi ya watumishi wa Mahakama na kuhamishiwa kwa mashauri yote ya migogoro ya ardhi katika Mahakama kuanzia ngazi ya mwanzo hadi juu, badala ya mabaraza ya ardhi, ili kuondoa mkanganyiko wa kisheria.
Alisema Mahakama iko tayari kushirikiana na Wizara husika na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuandaa marekebisho ya kisheria yatakayowezesha utekelezaji wa mapendekezo hayo.

