Na Lucy Ngowi
RAIS wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Dkt. Suleiman Ikomba, amesema kuwa nafasi ya mwalimu haijikiti tu kwenye kufundisha darasani, bali pia inahusisha kulea maadili, kujenga uzalendo na kuwa kielelezo bora kwa kizazi kijacho.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Dkt. Ikomba ameeleza kuwa jukumu la mwalimu linazidi mipaka ya maandalizi ya masomo, kwani linahusisha kujenga jamii yenye nidhamu, utu na uwajibikaji.
Akizungumzia mchango wa CWT, amesema chama hicho kinaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha walimu wanadumisha hadhi ya kuwa mfano wa kuigwa katika jamii.
Amefafanua kuwa, chama kinaweka mkazo katika kuimarisha maadili ya taaluma ya ualimu kupitia mikutano, semina na majadiliano ya kitaaluma kwa wanachama wake, ili kuwakumbusha wajibu wao kwa wanafunzi, jamii na taifa.
Aidha, amebainisha kuwa CWT inashirikiana na mamlaka husika kukuza taaluma ya walimu, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wao katika kufundisha na kulea kwa weledi zaidi.
Pia amesisitiza umuhimu wa walimu kuzingatia uwajibikaji na nidhamu ya kazi, akieleza kuwa mwalimu mwenye maadili na ujuzi wa hali ya juu huwa kielelezo cha jamii nzima.
Dkt. Ikomba amehitimisha kwa kusisitiza kuwa lengo kuu la chama hicho ni kuhakikisha mwalimu wa Tanzania anapata heshima stahiki, anawajibika ipasavyo na anakuwa mfano bora kwa wanafunzi pamoja na jamii kwa ujumla.

