Na Lucy Lyatuu ,Dodoma
SERIKALI imeipongeza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa juhudi zake za kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana wenye ulemavu, na kwamba hatua hiyo inaendelea kufungua fursa za ajira.
Imesema utaratibu huo unawezesha vijana wengi kuchangia maendeleo ya taifa kupitia ujuzi wa kazi.
Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya utumishi katika viwanja vya Chinangali Park Dodoma, Waziri Wa Nchi,Ofisi Ya Waziri Mkuu, Tawala Za Mikoa Na Serikali Za Mitaa, (OWN-TAMISEMI) Prof. Riziki Shemdoe, amesema mafanikio ya kijana Joseph ambaye ni mlemavu ni ushahidi wa kazi kubwa inayofanywa na VETA.

Profesa Shemdoe alimwakilisha Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka, ambapo alipata bahati ya kukutana na kijana Joseph katika banda la VETA na kubainisha kuwa
Serikali imevutiwa na uwezo wa kijana mwenye ulemavu aitwaye Joseph aliyepata mafunzo kupitia VETA na kubobea katika usanifu wa majengo kwa kutumia mifumo ya kompyuta.

Amesema mafanikio ya Joseph ni ushahidi wa kazi kubwa inayofanywa na VETA katika kuwajengea vijana stadi za maisha na kuwaandaa kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali.
“Nimepata nafasi ya kuzungumza na kijana huyo wakati wa kutembelea mabanda mbalimbali ya maonesho na kujionea kiwango kikubwa cha ubunifu na utaalamu alionao katika kazi za usanifu wa majengo,” amesema na kuongeza.
“Nimezungumza naye kwa kina na nimejiridhisha kuwa ana uwezo mkubwa sana,huyu ni mfano wa vipaji vilivyopo nchini ambavyo vinahitaji kuibuliwa na kuendelezwa,naipongeza VETA kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwafikia vijana hawa na kuwapa stadi za maisha,”

Aidha Profesa Shemdoe amemuelekeza Katibu Mkuu wa Utumishi kuhakikisha Joseph anatafutiwa ufadhili wa masomo ili aendelee kujiendeleza katika taaluma ya teknolojia na usanifu wa majengo.
Hata hivyo , amesema ameelezwa kuwa kijana huyo kwa sasa anafanya kazi kupitia VETA kwa mkataba hivyo akaagiza kuanza kwa mchakato wa kumpatia ajira ya kudumu serikalini kutokana na uwezo aliouonesha.

