Na Lucy Ngowi
MAMLAKA ya Elimu na Ufundi Stadi (VETA) imetengeneza teknolojia ya udongo wa kuoteshea mazao ya bustani na mbogamboga ili kumpunguzia mkulima gharama za kilimo kwa lengo la kuongeza tija katika kilimo na jamii kwa ujumla.
Ofisa Ufuatiliaji na Tathmini ya Mafunzo VETA, Joseph Kimako amesema hayo
kwenye maonesho ya wakulima, wafugaji na Wavuvi yanayoendelea Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Amesema wanaonyesha teknolojia hiyo kwa kuwa udongo huo wa kuoteshea unaouzwa maduka ya kilimo umekuwa ukitoka nje ya nchi hivyo kuuzwa kwa gharama kubwa.
“Teknolojia hii ni rahisi ambapo tunachukua udongo wa msituni tunachanganya na samadi ya ng’ombe na pumba za mpunga na baada ya hapo tunawekwa kwenye mtambo unaochemsha maji ili kuua masalia ya magugu na wadudu.”amesema.
Amesema udongo kama huo unaouzwa kwenye maduka ya pembejeo unatoka nje ya nchi lakini virutubisho vinavyopatikana ndani yake ,vipo kwenye malighafi zinazopatikana hapa nchini.
“Kwa hiyo hili ni moja ya zao ambalo linapatikana kwenye fani zetu tatu za kilimo tunazozitoa VETA ambazo ni fani ya zana na mitambo ya kilimo ,fani ya mazao ya bustani na fani ya uzalishaji kwenye kilimo.”amesema.
Kwa mujibu wa Kimako ,wameamua kwenda na teknolojia hiyo kwenye maonesho hayo kuonesha udongo huo unapatikana hapa nchini.
Amesema sababu za kutengeneza teknolojia hiyo ni kumsaidia mkulima
aweze kupata mafunzo ya kutengeneza udongo huo ili alime kwa tija.
Amewashauri wakulima kwenda VETA kujifunza namna nzuri ya kutengeneza udongo huo ili kupunguza gharama za kwenye kilimo lakini mwisho wa siku watalima kwa tija.