Na Lucy Ngowi
RAIS wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya amesema waandishi wa habari wana nafasi kubwa ya kuelimisha jamii kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi mbalimbali za umma na binafsi, ikiwemo Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).
Nyamhokya ameitoa kauli hiyo wakati akifungua mafunzo kuhusu fidia kwa wafanyakazi kwa wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanaofanya Kazi katika Vyombo vya Habari (JOWUTA), yaliyofanyika jijini Dar es Salaam Mei 25, 2026.
Amesema mafunzo hayo yameandaliwa kwa ushirikiano na WCF kwa lengo la kuongeza uelewa kwa wanahabari kuhusu haki, mafao na taratibu za fidia kwa wafanyakazi ili waweze kuripoti masuala hayo kwa usahihi kwa umma.

Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa WCF, John Mduma, Nyamhokya ameishukuru JOWUTA kwa juhudi zake za kuwaunganisha wanachama na kuwajengea uwezo kupitia mafunzo hayo muhimu.
Ameeleza kuwa WCF ni taasisi ya hifadhi ya jamii iliyoanzishwa kwa mujibu wa sheria kwa ajili ya kuwahudumia wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi wanaopata ajali, kuugua au kufariki kutokana na kazi zao.

Aidha, amesema mfuko huo unatoa mafao mbalimbali ikiwemo huduma za matibabu, fidia ya ulemavu wa muda na kudumu, msaada kwa wategemezi wa marehemu pamoja na huduma za utengemao.
Nyamhokya amewataka wanahabari kutumia taaluma yao kuwahamasisha waajiri kujisajili WCF na kuwasilisha michango kwa wakati, huku pia wakielimisha wafanyakazi umuhimu wa kujiunga na vyama vya wafanyakazi ili kuimarisha mshikamano katika kutetea haki na maslahi yao.


