Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: CHAMA cha Makandarasi na Watoa Huduma za Kikandarasi (TUCASA), kimeiomba serikali kuchukua hatua madhubuti kuzuia ucheleweshaji wa malipo kwa makandarasi wanaotekeleza miradi ya maendeleo nchini.
Msemaji wa TUCASA Harris Kapiga, amesema hayo alipozungumza na Waandishi wa Habari alipokuwa akielezea kuhusu kufanyika kwa kongamano lijulikanalo kama TUCASA Day 2025 litakalofanyika kuanzia Septemba mbili hadi tatu, mwaka huu, 2025 katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Kapiga ametaja mapendekezo mengine ya chama hicho ni pamoja na kutungwa kwa Sheria ya Malipo itakayolazimisha malipo kufanyika ndani ya muda maalum wa kisheria kwa miradi ya ujenzi.
Pia chama hicho kimetaka kuanzishwa kwa Dhamana ya Malipo, ambapo taasisi zote za serikali zinazotoa mikataba ya ujenzi zitoe dhamana kwa makandarasi ili kuondoa mashaka ya kucheleweshwa kwa fedha.
“TUCASA pia imeitaka serikali kuanzisha sera maalum za kuongeza ushiriki wa wakandarasi wa ndani katika miradi mikubwa ya kitaifa ili kupunguza utegemezi kwa wakandarasi wa nje,” amesema.
Msemaji wa huyo wa TUCASA, Kapiga amesema hadi sasa deni kwa makandarasi limefikia Sh. Trilioni 1.20, ambapo makandarasi wa ndani wanadai Bilioni 190, kati ya hizo Bilioni 115 ni kwa miradi iliyokamilika, na Bilioni 75 kwa miradi inayoendelea.
Akinukuu Kamati ya Bunge ya Miundombinu, amesema kufikia Februari 2025, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ulikuwa na deni la Sh. Trilioni 1.20, linalojumuisha malipo kwa wakandarasi wa ndani, wa nje, na riba ya ucheleweshaji wa malipo.
Kapiga amesema, “Makandarasi ndio msingi wa maendeleo ya miundombinu. Nyumba unayoishi, daraja unalopita, umeme unaotumia kuchaji simu, yote yana mkono wa mkandarasi. Ucheleweshaji wa malipo kwa makandarasi ni sawa na kusimamisha ujenzi wa taifa. Tunahitaji suluhisho la kitaasisi na kisheria,”.
Amesema kwa kipindi cha miaka minne, deni kwa makandarasi limekuwa likiongezeka sambamba na bajeti ya Wizara ya Ujenzi. Katika bajeti ya mwaka 2025/2026, Serikali imeidhinisha Sh. Trilioni 2.28 kwa Wizara ya Ujenzi ongezeko la asilimia 28 kutoka bajeti ya mwaka uliopita.
Kwa mwaka 2024 pekee, Sh. Bilioni 507.759 zilihusiana na miradi inayoendelea, huku Bilioni 652.213 zikiwa ni madeni ya miradi iliyokamilika lakini haijalipwa.
Kuhusu kongamano hilo ametaja kauli mbiu yake inayosema, ‘Makandarasi na Watoa Huduma Wazawa ni Nguzo ya Uchumi wa Taifa’.
Mkutano huo utawakutanisha makandarasi na watoa huduma kutoka maeneo mbalimbali nchini kujadili changamoto zinazowakabili, ikiwa ni pamoja na ucheleweshwaji wa malipo, mikataba yenye masharti magumu, na utegemezi wa makandarasi wa nje.