Na Lucy Lyatuu,Morogoro
MFUKO Wa Utamaduni Na Sanaa Tanzania umesema mpaka sasa umetoa jumla ya mikopo yenye thamani ya sh bilioni 14.7 kwa miradi ya sanaa ipatayo 1386 katika mikoa 22 ya Tanzania Bara.
Ofisa Mtendaji Mkuu kutoka Mfuko huo,Nyakaho Mahemba amesema hayo katika tamasha la nne la Taifa la Utamaduni linalofanyika mkoani Morogoro na kuongeza kuwa kwa mkoa huo imetolewa mkopo wa sh milioni 807 kwa miradi ya sanaa ipatayo 93.

Amesema mfuko wa utamaduni na sanaa una jukumu la kuinua ubora wa kazi za wasanii,habari utamaduni na sanaa ili ziweze kujiendesha kibiashara kuzalisha ajira pamoja na kuchangia pato la Taifa.
“Mfuko unahudumia sekta kuu tatu ikiwemo habari,utamaduni ma sanaa,lakininpia ukitoa huduma kwa mtu mmojammoja,vikundi na kampujo,”amesema Mahemba na kuongeza kuwa katika utamaduni wanahudumia lugha pamoja na fasihi.
Kuhusu habari amesema unahusisha vyombo vya habari,watenengeneza maudhui na vyombo vya habari na kwa upande wa sanaa wanahudumia sanaa za maonesho,filamu,muziki pamoja na ufundi.



Amesema kuna huduma kuu tatu ya mkopo wa masharti nafuu,mafunzo na huduma nyingine ya ruzuku.Na Katika mikopo wanatoa kuanzia sh 200,000 hadi sh milioni 200 na riba ikiwa asilimia tisa ambayo inatozwa katika salio la mkopo.
Amesema pia wana muda wa rehema kuanzia miezi na rejesho ni mpaka miaka mitatu na kwamba Mfuko unatoa mafunzo mbalimbali na elimu ya fedha,urasimishaji na ujuzi.
“Hela ipo,mheshimiwa Rais ameweka fedha nyingi hivyo ni jukumu la wasanii na waandishi wa habari kukimbilia fursa hiyo ili kunufaika,”amesema na kuongeza kuwa serikali imedhamiria kukuza uchumi wa makundi hayo na kuwataka pia kufanya marejesho kwa wakati kwa wale ambao tayari wamenufaika ili kuwa na uendelevu wa mfuko na kukuza uchumi.
Kwa upande wake mnufaika wa mkopo kutoka Mfuko huyo ambaye ni Malkia Wa Taarab mkoa wa Morogoro, Amina Kidevu amewataka wasanii kutumianfursa ipatikanayo kutokana na mfuko huo ili waweze kujikwamua kiuchumi.

” Mkoa Wa Morogoro tayari tumepata mkopo kwa wasanii 50 wenye thamani ya sh milioni 800,hivyo waliokopa wafanye kazi kwa bidii ili kurejesha mkopo,amesema na kuongeza kuwa yeye tayari amenufaika kwa awamu mbili.


