MFANYAKAZI TANZANIAMFANYAKAZI TANZANIA
  • Home
  • Habari
  • Mfanyakazi
  • Magazeti
  • Bookmarks
Search
Magazeti
  • Home
  • Habari
  • Mfanyakazi
  • Magazeti
  • Bookmarks
Habari Mpya
  • Home
  • Habari
  • Mfanyakazi
  • Magazeti
  • Bookmarks
Chagua hapa
  • Home
  • Habari
  • Mfanyakazi
  • Magazeti
  • Bookmarks
  • Advertise
© 2024 Mfanyakazi Tanzania. All Rights Reserved.
Reading: Teknolojia Ya SmartShamba Planter Yageuza Dakika 30 Kuwa Tumaini La Mkulima
Share
Notification Show More
Font ResizerAa
Font ResizerAa
MFANYAKAZI TANZANIAMFANYAKAZI TANZANIA
  • Home
  • Habari
  • Mfanyakazi
  • Magazeti
  • Bookmarks
Search
  • Home
  • Habari
  • Mfanyakazi
  • Magazeti
  • Bookmarks
Follow US
© 2022 Mfanyakazi Tanzania. All Rights Reserved.
MFANYAKAZI TANZANIA > Tovuti > Makala > Teknolojia Ya SmartShamba Planter Yageuza Dakika 30 Kuwa Tumaini La Mkulima
Makala

Teknolojia Ya SmartShamba Planter Yageuza Dakika 30 Kuwa Tumaini La Mkulima

Lucy Ngowi
By Lucy Ngowi
Share
11 Min Read
Na Lucy Ngowi
Mkulima anapochelewa kupanda, si muda pekee unaopotea; anaweza pia kupoteza fursa ya kupata mavuno mazuri.
Kwa mkulima mdogo anayezitegemea nguvu kazi za familia au huduma za mashine zenye gharama, kuchelewa kwa upandaji kunaweza kuwa mwanzo wa hasara.
Tatizo hilo ndilo lililomsukuma kijana Ibrahim Meshack kugeuza changamoto ya shamba kuwa suluhisho la kiteknolojia, SmartShamba Planter, mashine inayolenga kurahisisha upandaji, kuweka mbegu kwa nafasi iliyopimwa, kupunguza muda na gharama na kuongeza tija.
Kwa Ibrahim, swali lilikuwa moja: Je, mkulima mdogo anaweza kupata teknolojia ya upandaji inayolingana na mazingira ya shamba lake bila kutegemea trekta kubwa na gharama kubwa?
Jibu lake limeanza kujengwa kupitia SmartShamba. “Lengo letu kubwa ni kuongeza uzalishaji wa mazao na kumwezesha mkulima kuongeza kipato. Ndiyo maana tumeendelea kuboresha mashine hii ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi, kupunguza muda wa upandaji na kuwafikia wakulima wengi zaidi,” anasema.
Kwa miaka mingi, wakulima wamekuwa wakitumia njia za kawaida, ikiwamo kupanda kwa mikono. Kwa shamba kubwa, njia hiyo inaweza kutumia muda mwingi na kufanya iwe vigumu kuhakikisha mbegu zinawekwa kwa nafasi na idadi inayotakiwa.
Ibrahim anasema SmartShamba imebuniwa kwa kuzingatia mazingira halisi ya mashamba ya wakulima wadogo, yakiwamo maeneo yenye mwinuko na yasiyo na usawa.
Hivyo, ubunifu huo haukuanzia kwenye teknolojia iliyopo na kutafutiwa matumizi, ulianzia kwenye tatizo la mkulima.
Ndipo SmartShamba ilipoanza tatizo la kawaida likageuzwa kuwa suluhisho la kiteknolojia.
Habari Picha 13432
Dakika 30 badala ya saa moja na nusu
Safari ya SmartShamba haikuishia kwenye wazo. Ibrahim anasema mashine hiyo ilianza kwa majaribio ya awali na baadaye ikaendelea kufanyiwa majaribio katika mashamba ya wakulima.
Kwa mujibu wake, imefanyiwa majaribio katika zaidi ya ekari 50 na tangu mwaka uliopita 2025 imetumika kupanda zaidi ya ekari 150.
Moja ya hoja kuu ni kasi. Ibrahim anasema SmartShamba inaweza kupanda ekari moja kwa takribani dakika 30, ikilinganishwa na karibu saa moja na nusu kwa trekta katika utaratibu wa kawaida.
Gharama nayo inalengwa kupungua. Kwa makadirio yaliyotolewa na mbunifu, matumizi ya SmartShamba yanakadiriwa kufikia takribani Sh35,000 kwa ekari, ikilinganishwa na karibu Sh60,000 kwa ekari kwa trekta.
Mashine hiyo inahitaji watu wawili wakati wa upandaji, mwendesha mashine na mhudumu anayesimamia uwekaji wa mbegu na mbolea pamoja na kufuatilia mchakato.
Kwa sasa, bei yake inakadiriwa kuwa kati ya Sh milioni tatu hadi tano, huku lengo likiwa kushusha gharama hiyo hadi chini ya Sh. milioni tatu baada ya uzalishaji kufanyika kwa wingi.
Habari Picha 13433
Nafasi iliyopimwa, ufanisi zaidi
Kwa COSTECH, thamani ya SmartShamba haipo kwenye kasi pekee.
Taasisi hiyo imeeleza kuwa ubunifu huo unaweza kuongeza ufanisi kwa kupunguza utegemezi wa upandaji wa mbegu kwa mikono na kuhakikisha mbegu zinawekwa kwa nafasi zilizopimwa kisayansi.
SmartShamba pia inaweza kusukumwa na mtu au kutumia wanyama kama ng’ombe, hivyo kuongeza uwezekano wa kutumika katika mazingira mbalimbali ya kilimo.
Hilo linaifanya teknolojia hiyo kuendana na uhalisia wa mkulima mdogo ambaye anaweza kuwa na shamba dogo, lenye mwinuko au asiyeweza kumudu trekta.
Je, mavuno yanaongezeka?
Hili ndilo swali muhimu zaidi kwa teknolojia ya kilimo: si kama mashine inafanya kazi kwa haraka, bali kama inamsaidia mkulima kupata matokeo bora.
Kwa zao la mahindi, Ibrahim anaeleza kuwa kwa njia ya kawaida mkulima anaweza kupata takribani magunia saba hadi 15 kwa ekari, kutegemea mazingira, mbegu na usimamizi wa shamba.
Kwa kutumia SmartShamba, uzalishaji unalengwa kufikia magunia 25 hadi 35 kwa ekari pale mazingira na usimamizi wa kilimo vinaporuhusu.
Kwa mbaazi, anasema matumizi ya mashine hiyo yamehusishwa na uzalishaji wa takribani magunia sita hadi saba kwa ekari, kutoka karibu magunia matatu hadi manne kwa njia ya kawaida.
Hata hivyo, Ibrahim anaweka wazi kuwa mavuno hayawezi kuhusishwa na mashine pekee. Aina ya mbegu, mvua, mbolea, udongo na usimamizi wa shamba vina mchango mkubwa.
Katika jaribio moja, anasema shamba lililotumia SmartShamba lilipata wastani wa magunia 25, wakati eneo lililopandwa kwa njia ya kawaida lilipata wastani wa magunia nane.
“Upandaji ulifanyika kwa wakati mmoja na katika mazingira yanayofanana, lakini tofauti ilionekana katika uzalishaji. Hilo limetupa picha ya namna SmartShamba inavyoweza kusaidia kuongeza tija kwa mkulima,” anasema.
Hata hivyo, matokeo hayo bado ni sehemu ya majaribio na hayawezi kuchukuliwa kuwa kiwango cha mavuno kwa kila shamba.
Mkulima aonja tofauti
Kwa Lushii Martin, mkazi wa Mbulu mkoani Manyara, thamani ya SmartShamba inaonekana katika kazi ya kila siku.
“Napenda kutumia teknolojia hii kwa sababu inarahisisha kazi ya shamba. Inaokoa muda na inafanya kazi ya kupanda kuwa rahisi. Ninafurahia kuona teknolojia kama hii ikitengenezwa kwa ajili ya mkulima,” anasema.
Ushuhuda huo unaifanya SmartShamba ionekane si kama teknolojia ya maonesho pekee, bali kama chombo kinachotakiwa kuleta tofauti katika kazi halisi ya mkulima.
COSTECH yaipa nafasi
Safari ya SmartShamba ilifika katika programu za COSTECH baada ya Ibrahim kupata fursa ya kuwasilisha ubunifu wake kupitia Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU).
Kwa sasa, mchakato wa kuunga mkono ubunifu huo unaendelea. Kati ya watu 261 walioomba nafasi 30, waombaji 196 walifikia hatua iliyofuata na 34 wakafikia hatua ya pitching. Kati yao, 12 walifanikiwa kupita hatua hiyo, huku watano wakichaguliwa kupata msaada, wakiwamo wabunifu wa SmartShamba.
Msaada huo utatolewa baada ya maonesho na utahusisha ruzuku pamoja na msaada wa kitaalamu kwa lengo la kusaidia ubunifu huo kukua na kuendelezwa kibiashara.
Kwa COSTECH, SmartShamba ni mfano wa namna vijana wanavyoweza kutumia sayansi, teknolojia na maarifa yao kutatua changamoto zinazowakabili Watanzania.
Programu ya MAKISATU yenyewe inalenga kusaidia wabunifu kuendeleza bidhaa zao hadi kufikia hatua ya kuthibitishwa na kuwa tayari kibiashara, huku ikitoa msaada wa kitaalamu na kifedha.
Kutoka Kumbi ya Ubunifu ya Buni hadi soko
Katika safari hiyo, Kumbi ya Ubunifu ya Buni imekuwa sehemu ya simulizi ya kuunganisha ubunifu na fursa za kuukuza.
Promise Mwakale ni miongoni mwa waliotoa mtazamo kuhusu umuhimu wa ubunifu unaotokana na mahitaji halisi ya jamii.
Kwa SmartShamba, thamani ya safari hiyo haipo tu katika kutengeneza mashine, bali katika kuonyesha namna tatizo la mkulima linavyoweza kubadilishwa kuwa bidhaa inayoweza kutumika, kuuzwa na kuibua fursa nyingine za kiuchumi.
Habari Picha 13434
Wateja wapo, uzalishaji ndio mtihani
Ibrahim anasema tayari kuna wateja wanaohitaji SmartShamba, lakini uwezo wa kuongeza uzalishaji bado ni changamoto.
“Tayari tumepata wateja wanaohitaji bidhaa hii na tunatarajia kuendelea kuwauzia kadiri uzalishaji utakavyoongezeka. Lengo letu ni kuhakikisha SmartShamba inawafikia wakulima wengi zaidi na kusaidia kuongeza uzalishaji wao,” anasema.
Changamoto nyingine ni upatikanaji wa mbegu kwa wakati na kwa kiwango kinachohitajika.
“Changamoto nyingine ni upatikanaji wa mbegu. Wakulima wanapata shida kupata mbegu kwa wakati na kwa kiwango kinachohitajika. Hili ni moja ya changamoto ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi ili kupata matokeo bora,” anasema.
Hivyo, SmartShamba inalenga kutatua sehemu moja muhimu ya mnyororo wa uzalishaji na upandaji wakati changamoto nyingine zinahitaji suluhisho kutoka kwa wadau mbalimbali.
Kutoka wazo hadi fursa ya ajira
Kwa Ibrahim, kuongeza uzalishaji wa mashine hakutawanufaisha wakulima pekee. Anaona kuna uwezekano wa kuzalisha ajira kwa vijana katika uzalishaji, huduma na matumizi ya teknolojia hiyo.
“Tutahitaji vijana ambao watashughulikia mbegu na shughuli nyingine wakati wa upandaji. Hivyo tutakuwa tunatengeneza ajira na kuwapa vijana wa vijijini nafasi ya kupata kipato,” anasema.
Kwa mtazamo huo, SmartShamba inagusa zaidi ya kilimo. Inaunganisha sayansi, teknolojia, uzalishaji, biashara na ajira.
Mtihani mkubwa sasa ni kufika kwa mkulima
Katika miaka 40 ya COSTECH, hadithi ya SmartShamba inaonyesha safari ambayo ubunifu wa ndani unaweza kupitia: tatizo, wazo, mfano, majaribio, msaada wa kitaalamu na hatimaye soko.
Lakini safari hiyo bado haijafika mwisho.
Ibrahim tayari ameonyesha kuwa mashine inaweza kufanya kazi katika mazingira ya wakulima. Kuna ushahidi wa awali kuhusu kupunguza muda na gharama, pamoja na matokeo ya majaribio yanayoonyesha uwezekano wa kuongeza tija.
Sasa maswali makubwa yamehamia kwenye hatua inayofuata: Je, uzalishaji utaongezeka? Je, bei itashuka na kufikiwa na mkulima mdogo? Je, matokeo yataendelea kujirudia katika maeneo na mazingira tofauti? Na je, teknolojia hii itafikia wakulima wengi kiasi gani?
Majibu ya maswali hayo ndiyo yatakayoamua kama SmartShamba itabaki kuwa ubunifu wenye kuvutia au itageuka kuwa suluhisho lenye athari pana katika kilimo.
Kwa Ibrahim, hatua inayofuata ni kuongeza uzalishaji, kuendelea kuboresha mashine na kuwafikia wakulima wengi zaidi.
“Tunataka vijana wajue kwamba wanaweza kubuni vitu vinavyotatua changamoto zilizopo katika jamii. Tukiwajengea uwezo huo mapema, tutakuwa na kizazi cha wabunifu kitakachosaidia kulijenga taifa,” anasema.
Kutoka kwa mkulima anayepanda kwa mikono hadi mashine inayoweza kupanda ekari moja ndani ya takribani dakika 30, SmartShamba Planter imeanza safari ya kubadili namna upandaji unavyofanyika.
Sasa mtihani wake mkubwa si kama inaweza kubuniwa; ni kama inaweza kuzalishwa kwa wingi, kumudu gharama na kufika mikononi mwa mkulima anayehitaji suluhisho.
Hapo ndipo SmartShamba inapovuka mipaka ya kuwa mashine ya kupandia na kuwa mfano wa namna tatizo la ndani linavyoweza kuzaa teknolojia ya ndani na teknolojia hiyo ikageuka kuwa fursa ya kuongeza tija, kipato na ajira.
Habari Picha 13435

You Might Also Like

Barabara Zinazopasuka, Suluhisho Linalotoka Maabara za Tanzania

Shen Zhiying: Mkongwe Aliyeanzisha Kozi Ya Kiswahili Nchini China

Ukarabati wa Reli Ya TAZARA Wafungua Ukurasa Mpya China, Afrika

Vidukari Hatari Vyafuatiliwa Mikoa 17 Kulinda Zao la Mpunga

Martha Mariki Achukua Fomu Kutetea Nafasi Yake Katavi

Share This Article
Facebook Twitter Whatsapp Whatsapp Email Copy Link Print
Previous Article OUT: Elimu Sasa Kiganjani
Leave a comment Leave a comment

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Stay Connected

235.3kFollowersLike
69.1kFollowersFollow
11.6kFollowersPin
56.4kFollowersFollow
136kSubscribersSubscribe
4.4kFollowersFollow
- Advertisement -
Ad imageAd image

Latest News

OUT: Elimu Sasa Kiganjani
Habari Uncategorized August 24, 2026
NGARUMA VTC  Kutoa Mafunzo Katika Fani Mbalimbali Za Ufundi
Habari August 24, 2026
VETA kumpa nafasi Igobeko kuongeza ujuzi na kuwawezesha wengine
Habari August 23, 2026
Airtel Yajenga Darasa La Fursa Katika Shule Ya Sekondari Magaoni,Tanga
Habari August 23, 2026
//

To be acknowledged as Africa’s premier and most reliable digital media network, delivering exceptional content across all our platforms by 2025.

Sign Up for Our Newsletter

Subscribe to our newsletter to get our newest articles instantly!

MFANYAKAZI TANZANIAMFANYAKAZI TANZANIA
Follow US
© 2024 Mfanyakazi Tanzania. All Rights Reserved.
Welcome Back!

Sign in to your account

Lost your password?