Na Lucy Ngowi
SERIKALI kupitia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imesema itaendelea kutoa fursa za mafunzo ya ufundi kwa watu wenye mahitaji maalum na kugharamia ada zao, ikiwa ni sehemu ya kuwawezesha kupata ujuzi wa kujitegemea.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Anthony Kasore, amemtaka mhitimu wa kozi fupi ya useremala VETA Tanga, Ernest Igobeko, kujiandaa kuanza mafunzo Januari mwakani 2027, ili kuongeza ujuzi wake na baadaye aweze kuwasaidia na kuwafundisha watu wengine wenye mahitaji maalum.
Kasore ametoa maelekezo hayo wakati akizungumza na Igobeko, katika banda la VETA kwenye Maonesho ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayoendelea mkoani Tanga, ambaye ana mahitaji maalum na alikuwa akijifunza ujuzi wa kutengeneza vifaa.
“Jipange, Januari uanze masomo pamoja na mwalimu wako. Serikali itafanya utaratibu wa kukupatia ada kama ilivyo kwa wale walioanza mwaka huu, 2026” amesema.
Amesema mafunzo hayo yatamwezesha Igobeko kujifunza zaidi ya utengenezaji wa vifaa, ikiwamo matumizi ya mashine mbalimbali na kupata utaalamu wa kutengeneza vifaa vinavyoweza kuwasaidia watu wengine wenye mahitaji maalum.
Kasore amesema baada ya kukamilisha mafunzo hayo, Igobeko anaweza pia kupata fursa ya kuwa msaidizi wa mafunzo na kutumia ujuzi atakaoupata kuwafundisha wengine.
Amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira yatakayowawezesha watu wenye mahitaji maalum kupata fursa sawa katika elimu na mafunzo ya ufundi, ili waweze kutumia ujuzi wao kujitegemea na kuchangia katika jamii.

“Usikate tamaa. Kila kitu kinawezekana. Jipange kwa ajili ya mafunzo ili uweze kujifunza vitu vingi zaidi, kujua mashine mbalimbali na hatimaye uweze kuwasaidia wengine,” amesema.
Kwa upande wake, Igobeko amesema mafunzo aliyopata VETA yamemsaidia kuongeza kujiamini na kuonyesha kuwa watu wenye mahitaji maalum wana uwezo wa kufanya kazi za ufundi na kushiriki katika shughuli za maendeleo.
“Nawashukuru na kuwapongeza kwa sababu mmetupa nafasi ya kuonyesha uwezo wetu. Watu wenye mahitaji maalum kama sisi tunaweza kufanya kazi na kuchangia katika jamii badala ya kuwa tegemezi,” amesema.
Amesema mafunzo hayo yamemwezesha kupata ujuzi wa kutengeneza vifaa na kusaidia kubadili mtazamo wa baadhi ya watu waliokuwa wakiamini kuwa mtu mwenye ulemavu hawezi kufanya kazi za ufundi.
Igobeko amesema mafanikio hayo yameleta mabadiliko pia katika familia yake, baada ya kuona kazi anazoweza kufanya, jambo lililompa furaha na kuongeza hamasa ya kuendelea kujifunza.
Amesema anatarajia kutumia mafunzo atakayoanza Januari mwakani 2027 kuongeza ujuzi wa kutumia mashine mbalimbali na baadaye kuwasaidia watu wengine wenye mahitaji maalum kupata ujuzi na kujiamini.
Ametoa wito kwa watu wenye mahitaji maalum kutumia fursa zinazotolewa na Serikali katika mafunzo ya ufundi, akisema ujuzi huo unaweza kuwa msingi wa kujitegemea na kuchangia maendeleo ya jamii.

