Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM: MAMLAKA ya Elimu Tanzania ( TEA), iko mbioni kutafuta zaidi ya Sh. Bilioni 10 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kuwezesha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwenye takriban shule 500 za sekondari nchini ndani ya kipindi cha miaka mitano.
Aidha mamlaka hiyo imeungana na Ubalozi wa Uingereza pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa – Mpango wa Chakula katika kampeni ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia mashuleni.

Kaimu Mkurugenzi wa Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi ya Elimu wa TEA, Masozi Nyirenda amesema hayo katika warsha maalum iliyowakutanisha walimu wakuu, wapishi, na walimu wa lishe kutoka shule 50 za Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Warsha hiyo iliyofanyika katika Shule ya Msingi Liwati, imelenga shule zinazotarajiwa kufadhiliwa na WFP ili kuanza kutumia nishati safi ya kupikia.

Katika warsha hiyo, Nyirenda aliambatana na Kaimu Meneja wa Utafutaji Rasilimali na Hamasa wa TEA, Dkt. George Mofulu.
Nyirenda ametoa wito kwa wadau kushirikiana na mamlaka hiyo kufadhili mradi huo ili kutunza mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji.

Kwa upande mwingine, Balozi wa Uingereza nchini, Marianne Young pamoja na Mwakilishi wa WFP nchini, Ronald Tran Ba Huy, wamepongeza Serikali kwa juhudi zake za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia mashuleni na kuahidi kuendelea kuunga mkono juhudi hizo.



