Na Lucy Ngowi
DODOMA: WADAU mbalimbali wa mnyororo wa thamani wa afya ya udongo, wamekutana kubaini changamoto zinazowakabili wakulima ikiwa ni pamoja na kuangalia njia sahihi, endelevu za kutatua.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Dkt.Thomas Bwana akifungua mkutano wa wadau wa kilimo amesema, maabara hai ya afya ya Udongo inalenga kutatua changamoto mbalimbali za afya ya udongo.
Dkt. Bwana amesema lengo lake ni kumsaidia mkulima kupata tija bila kuingia gharama zisizo za lazima.
“Tukiwa na uhakika wa afya ya udongo maana yake tunaenda kumsaidia mkulima kutambua namna sahihi ya matumizi ya viuatilifu, mbolea na pembejeo nyingine hata aina ya zao linalofaa eneo husika,” amesema.

Naye Mratibu wa Mradi huo kutoka TARI, Dkt. Atugonza Bilaro amesema wilaya tatu za Tanzania Bara ikiwemo Kongwa na Babati Mkoa wa Dodoma, Mbozi mkoani Songwe, pamoja na Zanzibar katika visiwa vya Pemba na Unguja, ndiko mradi huo utakakofanyika.
Amesema mradi huo unakuja na njia husishi ya Maabara hai ya afya ya udongo ambayo inajumuisha wataalamu mbalimbali kutoka taasisi tofauti za umma na binafsi wenye lengo moja la kutatua changamoto za afya ya udongo ili kumuongezea mkulima tija.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Norwegian Institute for Bio economy Research (NIBIO), Profesa Udaya Sekhar, amesema suala la afya ya udongo ni muhimu katika kipindi hiki ambacho kumekuwa na changamoto mbalimbali zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.
Profesa Sekhar amesema kama suala la afya ya udongo halitaangaliwa kwa uzito unaostahili matokeo yake itapunguza tija na
kuhatarisha suala la usalama wa chakula.
TARI imewakutanisha wadau hao ikiwa ni
Hatua ya utekelezaji wa Mradi unaolenga kujenga uwezo wa kitaasisi kwa Watafiti na maofisa ugani, pamoja na mafunzo kwa wakulima juu ya afya endelevu ya udongo katika zama za mabadiliko ya tabianchi.
Mradi huo wa miaka minne kuanzia mwaka 2024 hadi 2027 unatekelezwa na TARI, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Zanzibar (ZARI, pamoja na NIBIO kwa ufadhili wa Shirika la maendeleo la Norway (Norad).