Na Lucy Lyatuu,Morogoro
NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kaspar Mmuuya, amesema Serikali imeendelea
kurekebisha mila na desturi zinazoweza kuwa kikwazo kwa wanawake kumiliki ardhi,na kusisitiza umuhimu wa jamii kutambua kuwa ardhi ni rasilimali inayopaswa kutumiwa kwa misingi ya haki na usawa.
Mmuuya ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi katika Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni, linalomalizika mkoani Morogoro, akieleza kuwa maboresho katika sera hiyo yanalenga kuimarisha usawa na haki kwa makundi yote katika upatikanaji na umiliki wa ardhi.


Amesema serikali inachukua hatua kuhakikisha utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Ardhi ya Mwaka 2023 unaondoa ubaguzi wa kijinsia na kutoa fursa sawa kwa wanawake na wanaume katika umiliki na matumizi ya ardhi.
Amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kulinda na kutumia ardhi kwa tija, huku akisisitiza kuwa mabadiliko ya sera na mifumo ya utoaji huduma yanalenga kurahisisha upatikanaji wa haki za ardhi kwa wananchi bila kujali jinsia.
Naibu Waziri huyo amewataka watumishi wa Wizara ya Ardhi kuendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, akisisitiza kuwa hakuna rushwa wala visingizio katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Mnapata huduma kwa wakati. Nendeni ofisini, si kwa madalali,” amesema Mmuuya, akiwataka wananchi kutumia njia rasmi za kupata huduma za ardhi na kutoa taarifa pale wanapokumbana na vitendo vinavyokiuka taratibu.


Kwa upande wake Kamisha Msaidizi wa Ardhi mkoani Morogoro Idrissa Kayera amesema katika muda siku tano mkoani hapo amesaini na kutoa hati 829 na kati ya hizo hati 278 ninza wanawake.
Amesema mchakato wa utoaji hati unaweza kukamilika ndani ya siku moja iwapo vielelezo vyote viko sawa na kuhamasisha wananchi kuona umuhimu wa kuwa na miliki salama na kwamba kila kipande cha ardhi kiwe na hati.


Aidha amehamasisha pia umiliiki wa pamoja kuepusha changamoto kwenye mirathi katika jamii.


